TANAPA: Hakuna rushwa

LICHA ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kukiri kuanza uchunguzi kwa baadhi ya watendaji wa Shirika la H... thumbnail 1 summary
LICHA ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kukiri kuanza uchunguzi kwa baadhi ya watendaji wa Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA), wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, shirika hilo limetamba kuwa liko safi.
Hatua ya TAKUKURU kuwachunguza watendaji hao ilitokana na maombi waliyopewa na Wizara ya Maliasili na Utalii kufuatia Naibu Waziri wa wizara hiyo, Lazaro Nyalandu, kuwatuhumu baadhi ya watendaji akidai wanadhulumu na kutumika katika kulihujumu shirika hilo.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa simu, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Alan Kijazi, alikiri uchunguzi huo kuendelea kwa baadhi ya watendaji, lakini akabainisha kuwa hakuna vitendo vya rushwa.
“Ni kweli uchunguzi umeanza kwa baadhi ya watendaji kutokana na tuhuma za Nyalandu, lakini nikuhakikishie hakuna rushwa hata siku moja. Ujue haya mambo hatujakaa chini pamoja kuyaweka sawa,” alisema.
Kijazi aliongeza kuwa, wanangojea uchunguzi huo ukamilike, lakini akasisitiza kwamba hajui kama kuna mtendaji atabainika.
Katika tuhuma zake, Nyalandu alidai kuwa TANAPA ina harufu ya rushwa, na kwamba tayari wamewasiliana na TAKUKURU ili ifanye uchunguzi dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazowakabili na kuwachukulia hatua za kisheria watakaobainika.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, alizungumza na gazeti hili hivi karibuni na kukiri kuwa watajikita zaidi katika kuangalia mapato ya maliasili kwa ujumla.
Hata hivyo, alikataa kuzungumzia kwa undani suala hilo kutokana na kuhofia kuingilia kazi za uchunguzi.
Nyalandu alidai TANAPA ilifanya uonevu kwa kampuni ya kitalii ya Ahsante Tours ya mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ambayo ilifungiwa kuingiza wageni wake katika hifadhi za taifa kuanzia Novemba 17 kutokana na deni wanalodaiwa.
Nyalandu alielezea sababu za kutetea kampuni hiyo ya kizalendo, akisema kuwa hana maslahi yoyote na wamiliki ambao ni mtu na mumewe, na wala hawajui ila baada ya kufuatilia aligundua walikuwa wapagazi kwa kipindi cha miaka kadhaa kiasi cha kufanikiwa hata kuanzisha kampuni yao.
Aliwataja wamiliki hao kuwa ni Stella na Cuthberth ambao walifika ofisini kwake Dar es Salaam, akiwa hawajui na kumuelezea tatizo linalowakabili kwa TANAPA kuwafungia kuendelea kutoa huduma ndani ya hifadhi zao.
Alisema kampuni hiyo tayari ilikuwa inailipa TANAPA dola milioni mbili kwa mwaka na kwamba ni kampuni ya pili inayoongoza kupandisha wageni katika Mlima Kilimanjaro na imeajiri wafanyakazi 600, wote Watanzania.
Nyalandu aliongeza kuwa, mwaka juzi walikopa katika benki ya TIB kiasi cha dola milioni 1.3 ili kufanikisha ujenzi wa hoteli ya Weruweru River Lodge ambayo alisema ni moja kati ya zinazoongoza mkoani humo inayomilikiwa na wafanyabiashara hao.
Kwamba kutokana na mtikisiko wa uchumi na changamoto zilizosababisha baadhi ya wageni kuahirisha safari ikiwa ni pamoja na vurugu za Jumuiya ya Uamsho Zanzibar, Kampuni ya Ahsante iliikopa tena TANAPA kiasi cha dola 70,000.
Alisema kuwa deni hilo walikuwa wakilipa kila mwezi na sasa limebakia dola 39,000 walizoshindwa kulipa kwa miezi miwili mfululizo kutokana na mtikisiko huo.

Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com