Abiria Precision Air waongezeka kwa asilimia 13

SHIRIKA la Ndege la Precision Air, limeendelea kufanya vizuri katika sekta ya anga kwa abiria wake kuongezeka kwa asilimia 13 kwa kipind... thumbnail 1 summary


SHIRIKA la Ndege la Precision Air, limeendelea kufanya vizuri katika sekta ya anga kwa abiria wake kuongezeka kwa asilimia 13 kwa kipindi cha Aprili mwaka jana hadi Januari mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Allen Sharr, alisema kwa kipindi hicho, shirika hilo lilibeba abiria 750,762 ukilinganisha na abiria 663,636 mwaka juzi.
“Soko la usafiri wa anga la Tanzania limekuwa katika ushindani mkubwa kutokana na ujio wa mashirika mapya.
“Hata hivyo, shirika la Precision limekuwa likifanya vizuri kwa idadi ya abiria kuendelea kuongezeka.
“Tumepata mafanikio haya kutokana na huduma za kipekee tunazotoa kwa wateja wetu, kwenda na ratiba ya safari zetu na ukarimu wa Kitanzania unaofurahiwa na abiria,” alisema Sharra.
Sharra alibainisha kuwa shirika limeongeza idadi ya safari zake katika njia tofauti kama mkoani Mbeya, kupenyeza katika mikoa ya kusini iliyopokelewa na muitikio mkubwa na kuwa na idadi ya safari zake mara nne kwa wiki kwa kutumia dakika 90 kupitia ndege aina ya ATR 42.
“Uanzishwaji wa safari za jioni za Mtwara kutokea Dar es Salaam saa kumi jioni umerahisisha usafiri kwa abiria wanaosafiri kwenda na kurudi mkoani hapo pamoja na kurudisha safari za Kigoma Januari mwaka huu,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima


Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com