292 waruhusiwa kuvuna shamba la Sao Hill

na Asha Bani WAZIRI wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki amewaruhusu watu 292 ambao vibali vyao vilisitishwa Januari mwaka hu... thumbnail 1 summary


na Asha Bani
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki amewaruhusu watu 292 ambao vibali vyao vilisitishwa Januari mwaka huu, kuendelea na uvunaji katika shamba la Sao Hill.
Kagasheki ametoa ruhusa hiyo baada ya kujiridhisha kuwa watu hao walipata vibali hivyo kwa kufuata taratibu za uvunaji, kutokana na awali kuwepo kwa utata.
Kagasheki wakati alipotembelea wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, Januari 25 na 26, mwaka huu, ili kusikiliza kero zilizoko wilayani humo kuhusiana na shamba la miti la Sao Hill, aliahidi kufanyia kazi baadhi ya masuala yaliyojitokeza.
Kuhusu suala la vibali 292 vilivyotolewa katika msimu wa mwaka 2012/13 na kusitishwa wakati wa ziara yake, waziri amelifanyia kazi na kubaini kuwa matatizo na changamoto zilizojitokeza zilitokana na utendaji katika kipindi cha mpito, hususan mabadiliko ya utaratibu wa utoaji vibali vya uvunaji.
Hivyo wadau hao 292 ambao hawana vibali rasmi vilivyochapishwa kutokana na kutumika utaratibu wa zamani, wameruhusiwa kukamilisha taratibu na kupewa vibali rasmi vya uvunaji.
Ruhusa hii inawahusu wavunaji wote waliofuata taratibu zote za usajili, ikiwa ni pamoja na kupata usajili na kulipia maduhuli na tozo mbalimbali za serikali ambazo ndizo vigezo muhimu vya kumfanya mvunaji kufanya shughuli zake zinazohusiana na masuala yote ya uvunaji.
Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kufanyia kazi kero zote zilizojitokeza wakati wa ziara hiyo ya waziri na taarifa itaendelea kutolewa kuhusu utekelezaji wake.

Chanzo: Tanzania Daima

Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com