Manispaa Moshi yadaiwa kuhujumu uwanja wa ndege

na Rodrick Mushi, Moshi NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, amesema amefedheheshwa na kitendo cha uongozi wa manispaa ya Moshi kutak... thumbnail 1 summary

na Rodrick Mushi, Moshi
NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, amesema amefedheheshwa na kitendo cha uongozi wa manispaa ya Moshi kutaka kuua uwanja wa ndege wa Moshi kwa kugawa ardhi ya uwanja kwa baadhi ya watu.

Mbali na hilo alisema pia kuna mkanganyiko wa mchoro wa uwanja huo wa awali baada ya kubadilishwa.
Tizeba alisema hayo mjini hapa jana baada ya kufanya ziara yake kwenye uwanja huo akiwa ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Moshi, Philemon Ndesamburo.
Katika ziara hiyo walizunguka maeneo mbalimbali ya uwanja huo na kujionea ujenzi uliofanyika ndani ya uwanja huo.
Akizungumza kwenye kikao kilichofanyika ndani ya uwanja huo, Tizeba alisema kufa kwa uwanja huo kunachangiwa na watu wa Moshi wakiwemo baadhi ya viongozi wa manispaa.
Kutokana na hali hiyo alimtaka kufika Ofisa Mipango Miji, Alex Poteka, ambaye alifika muda mfupi huku majibu yake yakionyesha kutomridhisha naibu waziri huyo.
Awali akitoa malalamiko kwa Waziri Tizeba, meneja wa uwanja huo wa ndege, Francis Massao, alilalamika kuomba michoro ya awali ya uwanja huo toka kwa uongozi wa manispaa akiwamo ofisa mipango miji, Poteka, kwa kuandika barua bila mafanikio.
“Hivi ni wapi au ni uwanja gani wa ndege unaoweza kuongoza ndege huku kukiwa kuna nyumba imejengwa katikati ya uwanja!?” alisema Massao.
Tizeba alisema kuwa uwanja wa Moshi ni uwanja mkongwe kuliko yote ila umechoka kutokana na kutofanyiwa ukarabati muda mrefu.
Kwa upande wake, Poteka alijitetea kuwa hana taarifa kamili juu ya watu waliojenga kwenye eneo hilo la uwanja.

Chanzo: Tanzania Daima

Una taarifa, picha za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii? tutumie kupitia kingkahindi@gmail.com