Makaburi yachelewesha upanuzi wa JNIA

Sababu za kucheleweshwa kwa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, zimeelezwa kuwa ni kutokana na uwapo wa maka... thumbnail 1 summary
Sababu za kucheleweshwa kwa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, zimeelezwa kuwa ni kutokana na uwapo wa makaburi ndani ya eneo husika.
Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Uchukuzi,Dk Charles Tzeba,wakati akijibu swali la Abbas Mtemvu (Temeke-CCM),aliyetaka kujua ni lini ujenzi wa uwanja huo katika eneo la Terminal 3 utakamilika.
Naibu waziri huyo alisema kuwa,kucheleweshwa kwa upanuzi huo kulitokana na Serikali kutaka ilipe kwanza kifuta jasho kwa wanandugu wa wafu waliozikwa katika maeneo hayo jambo ambalo limekamilika Oktoba 8,mwaka huu.
Alisema kazi ya ujenzi wa uwanja huo inatarajiwa kuanza Januari,2014 na kukamilika Oktoba 2015 na itafanyika kwa awamu mbili.
Kwa mujibu wa Tzeba,awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa jengo la abiria na usimikaji wa mitambo mbalimbali kama vile mifumo ya ulinzi na usalama, habari na mawasiliano na maeneo ya kubebea mizigo.
Alieleza kuwa jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 3.5 kwa mwaka pamoja na maegesho ya ndege na madaraja yatakayokidhi ndege kubwa tano aina ya B777-300ER.
Kuhusu awamu ya pili alisema,itahusisha ufungaji wa mitambo ya kuhudumia abiria milioni 2.5 kwa mwaka na maegesho ya ndege yatapanuliwa ili kuweza kuegesha ndege kubwa ya abiria aina ya Airbus 380.
Alisema pia mradi huo utakapokamilika,Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,utaweza kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka na kuegesha ndege zote kubwa hata aina ya Airbus A380.

Chanzo: Mwananchi