Very hot: Maeneo 10 ya kutembelea msimu wa Krismas na Mwaka Mpya

Kipindi hiki cha kuelekea sikuu kuu za Krismas na kuukaribisha mwaka mpya ni wakati wa hekaheka kwa kila mtu, ambapo hutumia muda h... thumbnail 1 summary


Kipindi hiki cha kuelekea sikuu kuu za Krismas na kuukaribisha mwaka mpya ni wakati wa hekaheka kwa kila mtu, ambapo hutumia muda huu kununua zawadi kwaajili ya ndugu jamaa na marafiki, kufanya manunuzi na kujumuika pamoja na familia katika maeneo mbalimbali.

Watanzania wengi wamekuwa na shauku kubwa ya kutembelea hifadhi za Taifa na kuona vivutio vya utalii hapa nchini katika kipindi cha msimu wa siku kuu kama hizi lakini hushindwa kufanya hivyo kwa sababu kadhaa ikiwemo kukosa taarifa sahihi za maeneo yapi watembelee na kwa wakati gani.

Makala haya yanalenga kukupatia taarifa za maeneo kumi bora ya vivutio vya utalii yanayofaa kutembelea wakati huu wa sikukuu za krismas na mwaka mpya ikiwa kama ni matumizi sahihi ya likizo yako kwa kujumuika na familia yako katika utalii huu.

Tanzania inaorodha ndefu ya vivutio vya utalii ambavyo vinasimamiwa kikamilifu na Shirika la Hifadhi za Taifa la Tanzania (TANAPA) lakini kuna ambazo zinafaa kutembelewa wakati huu wa sikuu kuu ambazo ni pamoja na hifadhi ya Taifa ya Arusha, Katavi, Mikumi, Manyara, Ruaha, Rubondo, Serengeti, Saadan, Udzungwa na Kitulo.

Mikumi
Mikumi ni moja ya hifadhi mashuhuri na kubwa nchini Tanzania ambayo  ina ukubwa wa kilometa 3230 na ipo umbali wa kilometa 283 magharibi mwa Dar ea Salaam. Aidha hifadhi hii iko kaskazini ya mbuga ya Selouse na iko njiani unapoelekea katika hifadhi ya Udzungwa, Selouse na Ruaha kwa barabara kutoka Dar ea Salaam na Inapatikana katika Mkoa wa Morogoro.

Ndani ya hifadhi ya Mikumi kuna simba ambao huwa wanaonekana wakiwa katika himaya yao ambapo wanyama wengine wengi hukimbilia katika eneo la miombo nyakati za mvua ambako unaweza kuwaona katika safu za milima. Hapo makundi makubwa ya nyati katika ukanda wa miombo wanaweza kuonekana.

Kwa upande wa ndege, wakati wa mvua huongezeka na kufikia zaidi ya aina 300. 

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, nyakati hizi kunakuwepo na makundi ya ndege wahamiaji kutoka nchi za Ulaya na Asia ambayo, huungana na makundi ya ndege wakazi kama vili chole.

Makundi makubwa ya tembo, viboko, swala, pundamilia na nyumbu huonekana katika eneo hili.

Muda mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kati ya mwezi juni na Februari lakini katika kipindi cha mvua barabara nyingi za ndani ya hifadhi hazipitiki hivyo ni jambo jema kupata maelekezo ya hali ya barabara kabla ya kuamua kutembelea, lakini uzuri wake ni kwamba hifadhi hiyo inafikika wakati wote wa mwaka.

Serengeti
Hifadhi ya Serengeti ni eneo kubwa la savana na misitu kaskazini mwa Tanzania hasa katika mikoa ya Mara na Arusha ambapo kuna idadi kubwa ya wanyama pori. Serengeti inajulikana hasa kwa uhamaji wa kila mwaka wa zaidi ya milioni moja ya nyumbuwanaovuka mto Mara.

Ukiachilia mbali wanyama nyumbu pia kuna aina nyingi nyingine za wanyama kati yao "watano wakubwa" wanaovuta watalii wengi hapa nchini ambao ni, tembosimbachuifisikifaru na nyati

Muda mzuri wa hutembelea hifadhi hii ni kati ya mwezi Octoba na Desemba, japo unaweza kutembelea hata miezi mingine katika mwaka.

Katavi
Hifadhi ya Taifa ya Katavi, ina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 4471, iko juu ya uwanda mpana wa mafuriko kusini magharibi mwa Tanzania katika mkoa wa Katavi zamani Rukwa. Mandhari kuu katika hifadhi hii ni maeneo yenye maji maji  yenye majani, mimea mithili ya mitende pamoja na mto Katuma.

Katavi inasifika kwa kuwa na idadi kubwa ya Mamba na viboko na ni kawaida kuyaona makundi makubwa ya Tembo yakila majani kwenye mabwawa huku miili yao ikiwa imefunikwa na maji na magugu.

Hifadhi hii inafikiwa kwa ndege za kukodi kutoka Dar es Salaam na Arusha  na kwa Gari kutoka Mbeya na pia kwa kupitia mkoani Kigoma wakati wa kiangazi Mei-Octoba na kuanzia katikati ya Desemba hadi Februari.

Uzuri mwingine ni kwamba hifadhi hii inafikika pia kwa reli kutoka Dar es Salaam kupitia Tabora hadi mpanda na kwa gari kutoka Mpanda.

Arusha
Hifadhi ya Taifa ya Arusha ina ukubwa wa kilomita za mraba 328.4, iko umbali wa kilomita 62 (kiasi cha mwendo wa saa moja kwa gari) kutoka mji wa kitalii wa Arusha.

Ikumbukwe kuwa hifadhi hii ni maarufu kwa wanyama jamii ya tumbili wajulikanao kama Mbega weusi na weupe. Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hii ni pamoja na Twiga,pundamilia, Nyati na digidigi.

Unaweza kuwaona Chui wakibarizi katika vivuli vya matawi ya miti inayokingwa na maanguko ya maji huku makundi kadhaa ya batamaji yakitafuta wadudu katika maziwa ya Momella.

Zaidi ya aina 400 za ndege wamethibitika kupatikana ndani ya hifadhi hii.

Safari za miguu na kupanda milima Meru ni moja ya burudani muhimu katika hifadhi ambapo mpandaji anahitaji kati ya siku 3-4 za kupanda mlima.

Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kati ya mwezi Juni na Februari ingawa mvua inaweza kunyesha mwezi Novemba. Kuna maeneo ya malazi ndani ya hifadhi yenye hadhi tofautitofauti kama hoteli, nyumba za wageni na makambi ya kuweka mahema ingawa wageni pia wanawezakupata malazi eneo nje ya hifadhi katika mji wa Usa River na Arusha mjini.

Udzungwa.
Hifadhi hii ya Milima ya Udzungwa ina hazina nyingi za mimea, ndege na wanyama ambao hazipatikani sehemu nyingine duniani.

Kati ya aina sita za jamii ya nyani wanapatikana katika hifadhi hii, mbili hupatikana katika hifadhi hii pekee; Mbega mwekundu wa Iringa (Iringa red colobus Monkey) na Sanje Crested mangabey’’ ambaye alikuwa hajulikani hadi mwaka 1979 na ndege mbalimbali.

Kivutio kikubwa zaidi ni Mto Sanje ambao unatoa maporomoko ya maji yenye urefu wa mita zipatazo 170 yakianguka kupitia msituni na kutua mithili ya mianzo ya ukungu bondeni. Hifadhi hii inaweza kutembelewa muda wote wa mwaka japo wakati wa mvua barabara sio nzuri sana.

Ziwa manyara.
Hifadhi hii ya Taifa ya Ziwa Manyara ni maarufu kwa Simba wanaopanda miti na lipo ndani ya hifadhi ambayo ina ndege wengi zaidi ya aina 400 wanaovutia wakiwemo ndege aina ya Korongo ambao huonekana kama pazia kubwa jeupe.
Idadi kubwa ya wanafunzi hapa nchi wanatembelea hifadhi hii na kujionea maajabu yaliyopo ambapo ni pamoja na kujionea wanyama kama Simba, Nyati, Tembo, Nyani, Chui, Pundamilia, na wanyama wengine wanaokula majani na wanaona chemichemi za maji moto yanayobubujika kutoka ardhini bila kukauka kwa mamilioni ya miaka.

Hifadhi hii ipo umbali wa kilomita 126 kutoka Arusha mjini, na wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kuanzia mwezi June hadi Desemba.

Ruaha.
Hifadhi ya Ruaha ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania ambapo ina ukubwa wa kilomita za mraba 20,226 na ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Afrika baada ya hifadhi ya Kafue iliyopo nchini Zambia.
Ni maarufu kwa kuwa na wanyama aina ya Kudu wakubwa na wadogo ambao hupatikana kwa wingi ambapo ustawi wa hifadhi hii unategemea mto ruaha ambao aina mbalimbali za Samaki, Mamba na viboko hupatikana katika mto huu.

Wanyama kama Pofu na swala hunywa maji katika mto huo wa Ruaha ambao ni mawindo makubwa ya wanyama wakali wakiwemo Simba, Chui, Mbweha, Fisi na Mbwa mwitu. Pia eneo hili Tembo hukusanyika kwa wingi kuliko eneo lolote la hifadhi zilizopo katika nchi za Afrika Mashariki.

Katika hifadhi hii utajionea Magofu yanayosadikiwa kuwa yalikuwa makazi ya watu wa kale katika Kijiji cha Isimila kiasi cha Kilomita 120 kutoka Iringa. Magofu haya ni miongoni mwa historia ya kale barani Afrika.

Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ili kuangaliwa wanyama wakubwa ni wakati wa kiangazi kuanzia Mei hadi Desemba, lakini kuangalia ndege na maua wakati wa masika ni Januari –April .

Rubondo.
Hifadhi hii ya Taifa ni kisiwa ambacho kipo pembezoni mwa Ziwa Victoria, ziwa ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani likiwa linazungukwa na nchi Tatu, Tanzania, Uganda na Kenya.
Kisiwa hiki kinaundwa na visiwa tisa vidogo vidogo ambapo kisiwa hiki cha Rubondo ni makazi na mazingira muafaka ya kuzaliana Samaki wakiwemo Sato na Sangara wenye ukubwa wa uzito wa kilo hadi 100.

Wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni pamoja na Viboko,Pongo, Nzohe, Fisi maji, Mamba na Pimbi, wanabadilishana makazi na wanyama wengine waliohamishiwa katika hifadhi hii kama Sokwe, Tembo, Mbega weusi na weupe na Twiga.

Wakati mzuri wa kutembelea ni wa Kiangazi June-Agosti aidha wakati wa masika Novemba-Machi kwa ajili ya kuona maua na vipepeo na vile vile Desemba-Februari kwa kuwaona ndege wahamiaji.


Saadani.
Hifadhi hii ipo ufukweni mwa bahari ya Hindi na ni hifadhi pekee Afrika Mashariki inayoungana na Bahari na ipo umbali wa Kilomita 100 kaskazini Magharibi mwa Dar es Salaam na umbali kama huo kusini Magharibi mwa bandari ya Tanga.
Ilianzishwa kama pori la akiba mwaka 1960 na ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka 2005 na ukifika hapo unaweza kuona wanyama kama Simba, Chui, Fisi, Tumbili, swala na ngedele na mtalii mbali ya kuona wanyama pia unapata nafasi ya kuogelea na wakati wa kutembelea ni wakati wowote kwa mwaka ingawa wakati wa masika barabara zinaweza kutopitika kirahisi.

Kitulo.
Awali hifadhi hii ilijulikana kwa jina la Elton Plateau baada ya Mvumbuzi Fredrick Elton kupia eneo hili mnamo mwaka 1870, mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO)ilichukua eneo hili kwa ajili ya ukulima wa ngano na ufugaji wa Kondoo.
Baadaye likageuzwa kuwa shamba la Ng’ombe ambalo lipo hadi leo. Mwaka 2005 Kitulo likatangazwa kuwa hifadhi ya Taifa na ni hifadhi ambayo ina maua aina mbalimbali na zaidi ya aina 30 hupatikana Kitulo pekee.

Pia ndiyo eneo pekee Tanzania ambapo ndege aina ya Tandawala  machaka (Denhams Bustard) wana makazi na ndani ya hifadhi hii kuna miti aina ya Cidar yenye urefu wa zaidi ya mita 50 na inakadiliwa kuwa mirefu kuliko yote duniani.

Kitulo inafikiwa kwa gari kutoka Chimala kilomita 78 Mashariki mwa mji wa Mbeya. Reli ya TAZARA hupita karibu na hifadhi hii.

Huu ni muda muafaka kwa Watanzania kutumia fursa ya uwingi wa vivutio vya utalii nchini kujifunza na kupata ufahamu mkubwa wa uhifadhi na utunzaji wa Mazingira na utunzaji wa maliasili zetu kwa kufanya utalii wa ndani.

Dotto Kahindi ni mwandishi wa habari za usafiri wa anga, mazingira, maliasili na utalii, wasiliana nae kwa ushauri wa safari yako 0655361266