HOTUBA
YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHESHIMIWA BALOZI KHAMIS S. KAGASHEKI
(MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA
MWAKA 2012/2013
I. UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na Taarifa
iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyochambua Bajeti
ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bunge lako sasa lipokee na kujadili
Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka 2011/12 na Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake kwa mwaka
2012/13. Napenda nianze kwa kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake Mhe.
James Daudi Lembeli (Mb.) kwa kuchambua Taarifa ya Utekelezaji kwa mwaka
2011/12 na Mpango wa Bajeti wa Wizara yangu kwa mwaka 2012/13. Ushauri
wao umezingatiwa katika Bajeti hii.
2.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua na kunipa
fursa ya kuiongoza Wizara hii yenye dhamana ya kusimamia Rasilimali za
Maliasili na Malikale na kuendeleza Utalii. Namhakikishia kuwa
nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kwa kushirikiana na wadau wote
kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi hii zinalindwa na kuwanufaisha
watanzania wote.
3.
Mheshimiwa Spika, kwa majonzi makubwa, naungana na Wabunge wenzangu
kutoa pole kwa Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na wananchi wote kwa msiba uliotupata kutokana na
kuzama kwa meli ya MV Skagit tarehe 18 Julai,
2012.
Nawatakia ahueni wale wote walionusurika katika ajali hiyo na kwa wale
waliofariki namuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi,
Amin.
4.
Mheshimiwa Spika, hotuba yangu inajikita katika maeneo makuu manne kama
ifuatavyo:- Kwanza nitaelezea kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya Mwaka 2010-2015; Pili ni utekelezaji wa ahadi nilizozitoa
katika Bunge la Bajeti la mwaka 2011/12 pamoja na maagizo mbalimbali
yaliyotolewa na Bunge na Viongozi Wakuu wa Serikali; Eneo la tatu ni
changamoto zinazoikabili Wizara yangu katika kutekeleza majukumu yake
pamoja na Mikakati iliyopo; na Sehemu ya nne ni Mpango wa Utekelezaji na
Malengo ya Wizara kwa mwaka 2012/13.
II. UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010-2015
5.
Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka
2010-2015 imeelekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kutekeleza
yafuatayo:- kuziwezesha jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kunufaika
na rasilimali za wanyamapori na misitu; kuboresha mazingira ya makazi ya
watumishi wanaoishi kwenye mazingira magumu; kuweka utaratibu
shirikishi wa upandaji na uvunaji miti na udhibiti wa moto; kuboresha
miundombinu ndani ya Mapori ya Akiba, Hifadhi za Wanyamapori na Misitu;
na kuendeleza jitihada za kuhifadhi mazingira katika mbuga za wanyama,
misitu, fukwe za bahari na maziwa.
Aidha,
Wizara imetakiwa kuongeza msukumo katika maeneo yafuatayo:- kuendeleza
ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kuzalisha asali na nta kibiashara; kukuza
mwamko na kuendesha kampeni za kuwashawishi watanzania kujenga utamaduni
wa kutembelea vivutio vya utalii; na kupanua wigo wa aina za utalii kwa
kuendeleza utalii wenye kuhusisha utamaduni, mazingira na makumbusho.
6.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Ilani, Wizara imeendelea
kuhamasisha wananchi kushiriki katika uhifadhi na matumizi endelevu ya
rasilimali za wanyamapori. Aidha, imewezesha kuanzishwa na kuendelezwa
kwa maeneo 38 ya Jumuiya ya Hifadhi za Jamii (WMAs) na kufanya
matengenezo ya viwanja 12 vya ndege vilivyoko katika Hifadhi. Vilevile,
nyumba sita za watumishi kwenye Mapori ya Akiba Ibanda na Rumanyika
zimewekewa mfumo wa umeme.
7.
Mheshimiwa Spika, kampeni kwa njia ya sinema kuhusu upandaji miti
zimefanyika katika vijiji 22 katika wilaya za Bagamoyo, Kibaha, Kilosa
na Kisarawe na vijiji 18 vinavyozunguka misitu ya hifadhi Pugu na
Kazimzumbwi. Kamati za Wilaya 28 zimewezeshwa kuendesha vikao vya
uvunaji na kufanya doria katika misitu ya asili. Vilevile, Wizara
imejenga nyumba mbili za kuishi watumishi katika Shamba la Miti Mtibwa
na kutengeneza barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 1,120 kwenye
mashamba ya miti pamoja na kujenga madaraja 10 katika shamba la miti Sao
Hill.
8.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwezesha ufugaji nyuki ambapo
mizinga 602 ilitengenezwa na kutundikwa katika vituo vinne vya maonyesho
vya Manyoni (174), Handeni (158), Kondoa (200) na Buha (70). Aidha,
mizinga 200 imesambazwa katika maeneo ya: Sumbawanga (50), Mpanda (50)
na Mbarali (100). Vilevile, wafugaji nyuki 66 katika wilaya ya Kahama
wamepatiwa mafunzo kuhusu ubora na usalama wa asali.
9.
Mheshimiwa Spika, Wizara ilizindua Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni na
kuendelea kuhamasisha jamii kuanzisha vikundi vya utalii wa
kiutamaduni. Vikundi hivyo vimeongezeka kutoka 34 mwaka 2010/11 hadi 41
mwaka 2011/12. Vikundi hivyo ni kutoka katika mikoa ya Lindi, Mara,
Arusha na Dodoma. Vilevile, Wizara imefanya zoezi la kutambua na kuweka
kumbukumbu za Urithi wa kihistoria uliopo majini katika kisiwa cha
Mafia. Kazi nyingine za utekelezaji wa Ilani zimefafanuliwa katika aya
ya 9 hadi ya 11 katika Kitabu cha Hotuba kilicho mbele yenu.
III. UTEKELEZAJI WA AHADI ZILIZOTOLEWA WAKATI WA BUNGE LA BAJETI MWAKA 2011/12
SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI
(i) Utekelezaji wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori
10.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha 2011/12, Wizara imeendelea
kutekeleza Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 kwa
kukamilisha kanuni zifuatazo:- Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za
Wanyamapori (WMAs); Vitambulisho vya maafisa Walioidhinishwa;
Uthaminishaji wa Nyara; Hati za Ufifirishaji wa Makosa (Compounding); na
Amri ya kipindi Kisichokuwa cha Uwindaji. Aidha, rasimu za Kanuni tano
ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kanuni hizo zimeainishwa
katika aya ya 12 ya Kitabu cha Hotuba.
(ii) Ulinzi wa Wanyamapori, Maisha ya Watu na Mali Zao
11.
Mheshimiwa Spika, doria-siku (patrol man-days) 75,593 zilifanyika ndani
na nje ya Mapori ya Akiba ambapo watuhumiwa 1,981 wamekamatwa kwa
makosa mbalimbali na kesi 1,280 zimefunguliwa. Aidha, vituo viwili
vimejengwa katika Wilaya za Rombo (Ngoyoni) na Siha (Visa – West
Kilimanjaro) kwa ajili ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu. Ujenzi
wa kituo cha Nangurukuru kilichopo katika Wilaya ya Kilwa unaendelea.
Vilevile, Wizara imelipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi
walioathirika na wanyamapori wakali na waharibifu. Jumla ya wananchi
1,342 wanaomiliki ekari 2,148 za mazao walilipwa Shilingi 167,672,500
ikiwa ni kifuta jasho. Aidha, jumla ya Shilingi 15,300,000 zililipwa
ikiwa ni kifuta machozi kwa wananchi 42 waliojeruhiwa na wanyamapori
pamoja na familia za watu wanane waliouawa na wanyama hao. Ufafanuzi
zaidi kuhusu ulinzi wa wanyamapori na maisha ya watu umeoneshwa katika
aya ya 13 hadi ya 15 katika Kitabu cha Hotuba.
(iii) Ushirikishaji Jamii Katika Uhifadhi wa Wanyamapori
12.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Wizara imehamasisha jamii kuhusu
uhifadhi shirikishi wa wanyamapori ambapo maeneo matano ya Jumuiya za
Wanyamapori (WMAs) yameanzishwa. Aidha, WMAs 12 katika wilaya 12
zimepata jumla ya Shilingi 200,000,000 kutokana na mapato ya uwindaji wa
kitalii. Kazi nyingine zilizofanyika katika kuimarisha uhifadhi wa
wanyamapori zimeainishwa kwa kina katika aya ya 16 hadi 17 katika Kitabu
cha Hotuba.
(iv) Maduhuli
13.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Idara ya Wanyamapori ilikadiria
kukusanya Shilingi 24,168,751,574 kutokana na vyanzo mbalimbali. Hadi
Juni, 2012 Shilingi Bilioni kumi na tano, milioni sabini na nne, hamsini
na tatu elfu, mia tisa sabini na mbili (15,074,053,972) sawa na
asilimia 62 ya makadirio zilikuwa zimekusanywa. Vilevile, Mfuko wa
Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania ulikadiria kukusanya Shilingi
16,287,141,880. Hadi Juni, 2012 makusanyo yalifikia Shilingi
11,673,240,697 sawa na asilimia 72 ya makadirio. Fedha hizo zimeendelea
kutumika kwa shughuli za kulinda wanyamapori, utafiti na mafunzo, kutoa
elimu kwa umma na kukarabati miundombinu.
(v) Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori
14.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2011/12, Chuo cha Wanyamapori-Mweka kimedahili
wakurufunzi 502 wa kozi za muda mrefu. Aidha, Chuo kimesomesha Wakufunzi
saba wa Shahada ya Uzamivu, watatu Shahada ya Uzamili na wafanyakazi
wanne wa kada za Ukutubi, Uhasibu na Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano.
15.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha miundombinu, Taasisi ya Taaluma ya
Wanyamapori Pasiansi imejenga darasa moja, mabweni mawili na kukarabati
nyumba tisa za watumishi. Mwaka wa masomo 2011/12, idadi ya udahili
iliongezeka kutoka wakurufunzi 236 mwaka 2010/11 hadi 284. Aidha, Kituo
cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga
kimedahili wakurufunzi 200 ikilinganishwa na wakurufunzi 137 mwaka
2010/11.
(vi) Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)
16.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, TAWIRI imeendelea kufanya tafiti
kuhusu wanyamapori, mimea, nyuki na kupe wa nyuki katika sehemu
mbalimbali nchini. Matokeo ya tafiti hizo pamoja na maeneo yaliyohusika
ni kama ilivyoainishwa katika aya ya 22 hadi aya ya 25 katika Kitabu cha
Hotuba.
(vi) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
17.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12 Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
imekarabati barabara zenye jumla ya kilomita 420 na kununua malori
manne. Aidha, Michoro ya jengo la kitega uchumi mjini Arusha
imekamilika. Vilevile, Mamlaka imekamilisha ujenzi wa madarasa matatu ya
Shule ya Msingi Jema na ukarabati wa majosho matatu katika maeneo ya
Meshili, Olpiro na Ndiani na majosho hayo yanatumika. Ujenzi wa mabwawa
matatu katika maeneo ya Ngairishi, Kaitangteng na Eltulele unaendelea.
(viii) Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)
18.
Mheshimiwa Spika, Shirika limeimarisha Idara ya Himasheria kwa kujenga
vituo 11 vya askari katika hifadhi za Kitulo, Saadani, Mkomazi na
Arusha. Aidha, askari 100 wameajiriwa na magari 26 yamenunuliwa kwa
ajili ya shughuli za uhifadhi. Katika kuboresha miundombinu, barabara
zilifanyiwa matengenezo na nyumba 21 zimejengwa katika hifadhi
mbalimbali zilizo chini ya TANAPA. Kazi nyingine zilizotekelezwa na
TANAPA zimeainishwa katika aya ya 28 hadi ya 30 katika Kitabu cha
Hotuba.
SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI
(i) Sera na Kanuni
19.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, nakala 2,750 za kijitabu cha Tozo za
Misitu zimechapishwa na kusambazwa. Aidha, Wizara imempata mtaalam
mwelekezi atakayeratibu zoezi la kupitia Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka
1998.
(ii)Kuendeleza Ufugaji Nyuki
20.
Mheshimiwa Spika, Ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuendeleza ufugaji
nyuki, jumla ya mizinga 205 na mavazi ya kinga 90 yametengenezwa na
kusambazwa kwa vikundi 20 vya ufugaji nyuki katika wilaya ya Kahama na
vikundi 10 katika wilaya ya Magu. Kila kikundi kilipata mizinga nane na
jozi tatu za mavazi ya kinga. Aidha, kufuatia maonesho ya Nanenane
yaliyofanyika hapa Dodoma na kushindanisha wafugaji nyuki, Wizara ilitoa
mizinga 100 kwa mshindi wa kwanza na 60 kwa mshindi wa pili.
(iii) Vyuo vya Taaluma ya Misitu na Ufugaji Nyuki
21.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwezesha vyuo vya misitu na
ufugaji nyuki ambapo mwaka 2011/12 jumla ya wakurufunzi 218 walidahiliwa
ikilinganishwa na wakurufunzi 205 waliodahiliwa mwaka 2010/11.
Wakurufunzi waliodahiliwa ni kwa ajili ya Chuo cha Misitu Olmotonyi –
Arusha (150); Chuo cha Nyuki Tabora (38); na Chuo cha Viwanda vya Misitu
Moshi (30).
22.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI)
Moshi kimekamilisha kukadiria gharama za ujenzi wa Maktaba na Maabara
ambapo ujenzi utaanza mwaka 2012/13. Aidha, Ujenzi wa Bwalo la Chakula
unaendelea katika Chuo cha Ufugaji Nyuki Tabora na lipo katika hatua za
mwisho kukamilika.
(iv) Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
23.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania umeanza
kutekeleza majukumu ya kiutendaji yaliyokuwa yanafanywa na Idara ya
Misitu na Nyuki. Majukumu yaliyotekelezwa ni pamoja na:- kutoa elimu kwa
umma na uhamasishaji; kushirikisha wadau katika kuendeleza misitu;
upandaji miti; kuimarisha miundombinu; kusimamia misitu ya hifadhi; na
kuendeleza ufugaji nyuki. Aidha, sampuli 60 za asali zilikusanywa katika
wilaya 17 kwa lengo la kuhakiki na kudhibiti viwango vya ubora wa mazao
ya nyuki. Kati ya sampuli hizo, 40 zimepelekwa katika maabara teule
nchini Ujerumani.
24.
Mheshimiwa Spika, vituo vinne vya ufugaji nyuki viliwezeshwa kusimamia
makundi ya nyuki 1,056 na kuanzisha Manzuki mbili. Kazi nyingine
zilizotekelezwa katika maeneo hayo zimeainishwa katika aya ya 37 hadi
aya ya 42 ya Kitabu cha Hotuba.
(v) Kuimarisha Ukusanyaji wa Maduhuli
25.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli, Wakala
uliwawezesha watumishi 142 wa Halmashauri za Wilaya, Sekretarieti za
Mikoa na Wizara kushiriki mafunzo kuhusu taratibu na kanuni za
ukusanyaji wa maduhuli.
Hadi
Juni, 2012 Shilingi Bilioni hamsini na tisa, milioni mia sita sitini na
sita, sabini elfu na mia moja themanini (59,666,070,180) sawa na
asilimia 151 ya lengo zimekusanywa. Aidha, Mfuko wa Misitu Tanzania
umekusanya shilingi 3,338,377,101 kufikia Juni 2012, ikiwa ni asilimia
111 ya makisio ya shilingi 3,000,000,000. Kazi zilizotekelezwa na Mfuko
zimeainishwa katika aya ya 45 na 46 ya Kitabu cha Hotuba.
(vi) Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA)
26.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Mbegu za Miti uliendelea kuzalisha na kuuza
mbegu na miche ya miti. Hadi Juni 2012, mbegu za miti zilizouzwa ndani
na nje ya nchi ni kilo 9,262 kwa thamani ya Shilingi 90,612,665. Maelezo
ya kina kuhusu aina za mbegu, miche ya miti na fedha zilizopatikana
yamefafanuliwa katika aya ya 47 ya Kitabu cha Hotuba.
(viii) Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI)
27.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Taasisi imeanzisha tafiti juu ya
matumizi ya maji kwa miti ya mikaratusi katika maeneo ya Shinyanga,
Korogwe, Lushoto na Kibaha. Aidha, Taasisi imeendelea na utafiti na
uzalishaji juu ya bioteknolojia ya aina 16 za kloni za miti ya
mikaratusi inayofaa kupandwa katika maeneo mbalimbali nchini. Pia,
Taasisi inatafiti juu ya ukuaji wa jamii 81 za mikaratusi aina ya
pellita huko Sao Hill kwa lengo la kuwapa wadau wa misitu miti yenye
ubora unaotakiwa. Maelezo zaidi kuhusu tafiti zilizofanyika yanapatikana
katika aya ya 49 ya Kitabu cha Hotuba.
28.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mfuko wa Misitu Tanzania, TAFORI imeanzisha
mashamba darasa kwa ajili ya miti ya kuni na mkaa katika vijiji vya
Lubungo na Gwata vilivyopo katika Wilaya ya Morogoro Vijijini na
Kwang’andu na Kihangaiko Wilaya ya Bagamoyo.
SEKTA YA UTALII
29.
Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha maboresho ya Kanuni za Tozo ya
Maendeleo ya Utalii na matumizi yake yataanza mwaka 2012/13. Elimu
imetolewa kwa wadau kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Utalii ya mwaka 2008
hususan katika eneo la kujisajili na kulipia leseni za uendeshaji wa
biashara ya utalii. Mikoa iliyohusika ni Pwani, Iringa, Rukwa,
Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Mara na Dar es Salaam
ambapo jumla ya Wakala 640 wa biashara ya utalii wamepatiwa elimu.
30.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Wizara imetoa mafunzo ya kupanga
hoteli katika daraja kwa wataalamu 17 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar,
kati yao 15 walifaulu na kutunukiwa vyeti. Wataalamu waliofuzu
wanatambulika na wanaweza kufanya zoezi la kupanga hoteli katika daraja
kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, Wizara imefungua ofisi
za utalii Iringa kwa ajili ya Nyanda za Juu Kusini na Mwanza kwa ajili
ya Kanda ya Ziwa. Kufunguliwa kwa ofisi hizo ni fursa ya kuchochea
mpango wa kuendeleza utalii na kutangaza vivutio katika kanda hizo.
31.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara kupitia Idara ya Utalii
ililenga kukusanya Shilingi 3,433,872,661 kutokana na leseni mbalimbali
za Wakala wa biashara ya utalii nchini. Hadi Juni, 2012, jumla ya
Shilingi 3,765,959,717 zilikusanywa. Makusanyo hayo ni asilimia 109.7 ya
makadirio.
(i) Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)
32.
Mheshimiwa Spika, Bodi kwa kushirikiana na wadau imetayarisha na
kusambaza vielelezo mbalimbali vya utalii. Vielelezo hivyo ni pamoja na
majarida ya Tan Travel, Accommodation Guide, Selling Tanzania ,
Conference Directory, Savor, Dar Guide, Dar life na Tanga Tourism Guide.
Vilevile, Bodi ilichapisha kijitabu cha Utalii wa Utamaduni (Culture
Tourism Book), DVD na CD Rom za utalii.
Jarida
la “Hard venture Tourism” litakalokuwa linatolewa kila baada ya miezi
minne limechapishwa ili kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo kwenye
maeneo ambayo ni magumu kufikika kutokana na sababu mbalimbali. Toleo la
kwanza la jarida hilo limetolewa mwezi Agosti, 2012. Kazi nyingine
zilizotekelezwa na Bodi zimeainishwa katika aya ya 55 hadi 58 katika
Kitabu cha Hotuba.
(ii) Wakala wa Chuo cha Taifa cha Utalii
33.
Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa tarehe
10 Desemba, 2011, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi Kampasi mpya ya Wakala wa Chuo
cha Taifa cha Utalii inayoitwa Bustani, Jijini Dar es Salaam. Kampasi
inatarajia kujiendesha kibiashara ikiwa ni sehemu ya mafunzo. Chuo
kinatoa mafunzo katika ngazi ya Astashahada na Stashahada katika tasnia
ya Ukarimu na Utalii kwa viwango vya kimataifa. Utekelezaji wa majukumu
ya Chuo umeainishwa katika aya ya 60 ya Kitabu cha Hotuba.
SEKTA YA MAMBO YA KALE
34.
Mheshimiwa Spika, kufuatia kukamilika kwa mkakati wa kutekeleza Sera ya
Taifa ya Malikale, Wizara inafanya mapitio ya Sheria Na. 10 ya Mambo ya
Kale ya mwaka 1964 na marekebisho yake Na. 22 ya mwaka 1979 kwa ajili
ya kuandaa Sheria mpya ya Malikale.
35.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara imekamilisha Mpangokazi
wa ufukuaji wa Nyayo za Laetoli. Ili kujifunza mbinu bora za uhifadhi wa
nyayo zinazopatikana katika miamba iliyotokana na Volcano, Kamati ya
wataalam ilifanya ziara ya kimafunzo katika nchi za China, Korea ya
Kusini na Ujerumani. Aidha, maabara ya nchi ya Ujerumani imetoa fursa
kwa Tanzania kutumia maabara hiyo katika masuala ya utafiti na uhifadhi
wa Nyayo za Laetoli.
36.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji la
Taifa iliandaa na kurusha vipindi 10 vya televisheni kuhusu malikale
zinazopatikana kwenye maeneo ya Tongoni, Mapango ya Amboni na maeneo
mengine ya Utalii katika Mkoa wa Tanga kupitia kipindi cha Zamadamu.
Vilevile, Wizara ilishiriki katika mkutano Mkuu wa Kituo cha Kimataifa
cha Mafunzo ya Uhifadhi na Ukarabati wa Mali za Kiutamaduni (ICCROM)
uliofanyika Roma, Italia. Tanzania ilifanikiwa kupata uenyekiti wa
mkutano huo ambao utadumu kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Novemba,
2011.
37.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara iliboresha mazingira ya
vituo kwa kufanya ukarabati wa ofisi katika vituo vya Magofu ya Tongoni –
Tanga na Kunduchi - Dar es Salaam. Vilevile, Makumbusho ya Kaole -
Bagamoyo yalifanyiwa ukarabati na kuwekwa vioneshwa. Wizara katika
kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara ilifanya ukarabati wa
Makumbusho ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Magomeni, Jijini Dar
es Salaam. Aidha, vifaa vilivyotumiwa na Mwalimu J.K.Nyerere
vilikusanywa, kufanyiwa matengenezo na kuwekwa kama vioneshwa katika
Makumbusho hiyo.
(i) Uhifadhi wa Mali Kale
38.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2011/12, Wizara iliendelea na
ukarabati wa Gereza (Ngome ya Mreno), Kasri ya Makutani, Husuni Kubwa na
Husuni Ndogo katika eneo la Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara.
Ukarabati huo umefanyika kwa ushirikiano wa Programu ya Maeneo ya
Hifadhi za Bahari na Ukanda wa Pwani (MACEMP), UNESCO, Mfuko wa Balozi
wa Marekani wa Uendelezaji Urithi wa Utamaduni na ‘ World Monument
Fund’.
(ii) Uchimbaji wa Urani katika Pori la Akiba la Selous
39.
Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya Wizara yangu ya Mwaka 2011/12,
ilitolewa taarifa kuhusu Serikali kupeleka ombi UNESCO kuruhusiwa
kufanya mabadiliko ya mipaka kwa kuondoa eneo la Mkuju lililoko katika
Pori la Akiba Selous katika urithi wa dunia ili litumike kwa uchimbaji
urani. Hii ni kwa kutambua kuwa Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka
2009 imeruhusu uchimbaji wa madini ya urani, mafuta na gesi ndani ya
Mapori ya Akiba.
40.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuliarifu Bunge lako
tukufu kuwa, Mkutano wa 35 wa Kamati ya Urithi wa Dunia UNESCO
uliofanyika Paris, Ufaransa tarehe 19 - 29 Juni, 2011 ulijadili maombi
hayo na maamuzi kutolewa katika Mkutano wa tarehe 02 Julai, 2012. Kamati
ilitoa idhini ya kipekee na isiyokuwa ya kawaida (exceptional and
unique approval) ya kuruhusu kufanyika marekebisho ya Mpaka wa eneo la
Urithi wa Dunia kwenye Pori la Akiba Selous ili kuruhusu shughuli za
uchimbaji wa madini. Eneo lililoruhusiwa ni kilometa 215 za mraba,
ambalo likijumuishwa na eneo la kinga (buffer zone) ni sawa na asilimia
0.8 ya Pori la Akiba Selous.
41.
Mheshimiwa Spika, pamoja na eneo hilo kuondolewa katika Urithi wa
Dunia, bado limebaki kuwa eneo la Pori la Akiba Selous. Hivyo,
kilichopungua ni eneo la Urithi wa Dunia na sio ukubwa wa Pori la Akiba.
Sambamba na shughuli za uchimbaji urani tahadhari za kimazingira
zitaendelea kuchukuliwa na taasisi husika kabla, wakati na baada ya
uchimbaji.
(iii) Ukusanyaji wa Maduhuli
42.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara kupitia sekta ndogo ya
Malikale iliweka lengo la kukusanya shilingi 540,263,633. Mapato hayo ni
kutokana na wageni wanaotembelea vituo vya Mambo ya Kale pamoja na ada
za utafiti. Hadi Juni, 2012, Wizara ilikusanya shilingi 516,496,180 sawa
na asilimia 95.6 ya makadirio.
(iv) Shirika la Makumbusho ya Taifa
43.
Mheshimiwa Spika, Ninayo furaha kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa
majengo ya Mradi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni yaliyogharimu
takriban shilingi bilioni 11 yamekamilika. Majengo ya Mradi huu
yalizinduliwa rasmi tarehe 3 Desemba, 2011 na Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa
Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
44.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2011/12, Shirika limeandaa
maandiko saba ya utafiti. Tafiti mbili kati ya hizo zimeanza kufanyika,
ambapo utafiti wa athari za kusitishwa kwa Tawala za Jadi katika
tamaduni unafanyika Iringa na utafiti kuhusu uhifadhi wa mimea ya
Shubiri (Aloe) unafanyika Dar es Salaam katika kijiji cha Makumbusho.
Kazi nyingine zilizofanyika zimeainishwa katika aya ya 73 hadi 75 ya
Kitabu cha Hotuba.
UTAWALA NA RASILIMALI WATU
45.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, katika jitihada za kukabiliana na
upungufu wa watumishi, Wizara ilipewa kibali cha kuajiri watumishi 152
na taratibu za kuajiri zinaendelea. Watumishi 124 wa kada mbalimbali
walipandishwa cheo kwa kuzingatia Miundo ya Utumishi wa Umma. Aidha,
watumishi 20 walithibitishwa kazini na watumishi 46 walibadilishwa cheo.
46.
Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji,
Wizara iliwezesha watumishi 170 kuhudhuria mafunzo mbalimbali ambapo
watumishi 70 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi na 100 mafunzo ya muda
mrefu. Aidha, ili kuwaimarisha watumishi kimaadili, mada kuhusu maadili
zilitolewa kwa watumishi 117 katika Mkutano wa Watendaji Wakuu wa
Wizara, Watumishi 305 wa Makao Makuu na kwa watumishi 230 kwenye Semina
ya mafunzo ya ukusanyaji maduhuli. Mafunzo maalum ya maadili yametolewa
kwa wajumbe saba wa Kamati ya Maadili ya Wizara Aprili, 2012 Mkoani
Morogoro. Aidha, Wizara ina Baraza la Wafanyakazi na katika mwaka wa
fedha 2011/12, imefanya vikao viwili vilivyoshirikisha wajumbe 70 kila
kimoja. Maelezo kuhusu ustawi wa watumishi yako katika aya ya 78 ya
Kitabu cha Hotuba.
CHANGAMOTO KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KWA MWAKA 2011/12
47.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji
wa majukumu yake, Wizara ilikabiliwa na changamoto mbalimbali kama
ifuatavyo:
i. Uhaba wa watumishi, hususan katika Sekta za Wanyamapori, Misitu na Malikale;
ii. Upungufu wa nyumba na huduma duni za watumishi katika vituo vya nje vya Wizara;
iii. Uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za maliasili na malikale;
iv. Mwamko mdogo wa wananchi kushiriki utalii wa ndani; na
v. Miundombinu duni katika maeneo yenye vivutio vya utalii.
48.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na
changamoto hizo kwa kujenga uwezo wa vyuo vya Wizara wa kudahili na
kupata wahitimu wenye sifa; kuomba kibali cha ajira mpya; kujenga makazi
ya watumishi; kuboresha maslahi ya watumishi; na kuboresha miundombinu.
Aidha, Wizara inaongeza ushiriki wa wadau katika uhifadhi na matumizi
endelevu ya rasilimali na kuhamasisha utalii wa ndani.
MPANGO WA UTEKELEZAJI NA MALENGO KWA MWAKA 2012/13
SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI
49.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara itaendelea
kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori kwa kufanya mapitio ya
Kanuni zilizopo na kuandaa Kanuni mpya za kutekeleza Sheria ya Uhifadhi
wa Wanyamapori Na.5 ya 2009.
50.
Mheshimiwa Spika, Wizara itaanzisha Pori la Akiba Piti katika Wilaya ya
Chunya pamoja na kukamilisha uanzishaji wa maeneo sita ya WMAs. Maeneo
hayo yameainishwa katika aya ya 81 ya Kitabu cha Hotuba. Aidha, gawio la
asilimia 25 ya fedha zitokanazo na uwindaji wa kitalii kwa Halmashauri
za Wilaya 42 na WMAs 16 litaendelea kutolewa.
51.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13 Wizara itakamilisha uanzishwaji wa
Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania. Vilevile, miundombinu, vitendea kazi na
huduma zitaboreshwa katika mapori ya Akiba na Kikosi Dhidi ya Ujangili
pamoja na kuongeza uwezo wa kufanya doria kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.
(i) Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori
52.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/13, vyuo vya Taaluma ya
Wanyamapori vitadahili jumla ya wakurufunzi 1,074 kama ifuatavyo: Chuo
cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka wakurufunzi 550; Chuo cha Taaluma ya
Wanyamapori Pasiansi 324; na Kituo cha Mafunzo ya Usimamizi wa Maliasili
kwa Jamii - Likuyu Sekamaganga 200. Kazi nyingine zitakazotekelezwa na
vyuo hivyo zimeainishwa katika Aya ya 83.
(ii) Shirika la Hifadhi za Taifa, Tanzania (TANAPA)
53.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Shirika litaweka kipaumbele katika
kuendeleza miundombinu ya barabara katika Hifadhi za Katavi, Ruaha,
Mikumi na Saadani pamoja na kununua magari 10 kwa ajili ya hifadhi
mbalimbali. Vilevile, nyumba nane kwa ajili ya familia za watumishi,
daraja moja na “drifts” tatu zitajengwa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha.
54.
Mheshimiwa Spika, Shirika litaendeleza utalii wa kutembea kwa miguu,
kuanzisha utalii wa usiku na utalii wa tufe (baloon) katika Hifadhi za
Taifa Katavi, Ruaha na Mikumi na kuendelea kutangaza vivutio vya Utalii
kwa kushirikiana na wadau wengine.
(iii) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
55.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Mamlaka itaendelea kufanya matengenezo
ya barabara na ukarabati wa majosho ndani ya eneo la hifadhi, kununua
magari mawili kwa ajili ya doria na kuanza ujenzi wa jengo la kitega
uchumi Arusha. Ufafanuzi wa kazi zitakazofanyika umeainishwa katika Aya
ya 86 ya Kitabu cha Hotuba.
(iv) Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)
56.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Taasisi itaendeleza utafiti na
kuidadi wanyamapori nchini pamoja na kujenga maabara ya kisasa ya
utafiti wa nyuki. Tafiti zitakazofanyika zimeainishwa katika aya ya 87
ya Kitabu cha Hotuba.
SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI
57.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kupitia Sera
ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, kukamilisha Sera ya Taifa ya
Misitu ya mwaka 1998 na kufanya maboresho kwenye vifungu vya sheria.
Aidha, Wizara itapitia viwango vya ubora wa mazao ya nyuki na shughuli
za ufugaji nyuki katika wilaya za Kigoma, Kibondo na Kasulu. Kazi
nyingine zitakazofanyika ili kuhifadhi misitu na kuendeleza shughuli za
ufugaji nyuki zimeainishwa katika aya ya 89 katika Kitabu cha Hotuba.
(i) Vyuo vya Taaluma ya Misitu na Ufugaji Nyuki
1.
58. Mheshimiwa Spika, Vyuo vya Misitu na Ufugaji Nyuki vinatarajia
kudahili jumla ya wakurufunzi 251 katika mwaka 2012/13 kama ifuatavyo:
Chuo cha Misitu Olmotonyi (155); Chuo cha Ufugaji Nyuki Tabora (61) na
Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (35). Wizara itaendelea kuwezesha Vyuo
vya Misitu na Ufugaji Nyuki vilivyopo chini yake kutekeleza majukumu
yao. Ukarabati wa baadhi ya majengo na kuweka samani na majiko katika
Chuo cha Ufugaji nyuki Tabora utafanyika. Aidha, Chuo cha Viwanda vya
Misitu Moshi kitaanza ujenzi wa Maktaba katika mwaka huu wa fedha.
(ii) Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA)
59.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Wakala utaendelea kutoa huduma kwa
kuuza mbegu na miche ya miti pamoja na kutunza vyanzo 31 vya mbegu za
miti ya aina mbalimbali. Ufafanuzi kuhusu kiasi cha mbegu na aina ya
miche itakayozalishwa upo katika aya ya 91 ya Kitabu cha Hotuba.
(iii) Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI)
60.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13, Taasisi itaendelea kufanya tafiti
mbalimbali pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi. Aidha,
Taasisi itaendelea kushirikiana na wadau wa kikanda na kimataifa kwa
lengo la kuhifadhi na kuongeza ubora wa miti. Maelezo ya kina kuhusu
tafiti zitakazofanyika na wadau watakaohusika yako katika aya ya 92 na
93 ya Kitabu cha Hotuba.
(iv) Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
61.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Wakala utaandaa mipango ya usimamizi
wa hekta 453,000 za misitu katika misitu ya asili na mashamba 15 ya miti
ya kupanda. Aidha, tathmini kuhusu rasilimali za misitu kupitia mradi
wa National Forest Resources Monitoring and Assessment (NAFORMA)
itafanyika ili kumalizia vitalu 108 vilivyobaki.
Vilevile,
litafanyika zoezi la kuweka mipaka na maboya (beacons) kwenye misitu ya
hifadhi na mashamba ya miti pamoja na kusafisha njia za kuzuia moto.
Maelezo kuhusu kazi zitakazotekelezwa na Wakala yapo katika aya ya 95
hadi 100 katika Kitabu cha Hotuba.
SEKTA NDOGO YA UTALII
62.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ina
mpango wa kuendeleza jiji la Dar es Salaam kuwa kivutio cha Utalii.
Mpango Mkakati wa miaka mitano (2012 - 2017) ambao utaanza kutekelezwa
mwaka 2012/13 umeandaliwa. Aidha, Wizara itafanya mapitio ya Sera ya
Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 ili kukidhi mahitaji ya sasa.
63.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sheria ya Utalii ya mwaka 2008,
Kanuni za Tozo za Maendeleo ya Utalii (Tourism Development Levy)
zimekamilika. Mwaka 2012/13, Wizara itahamasisha wadau kuhusu tozo hizo
na kuanza kutumika rasmi. Vilevile, Wizara itafanya utafiti wa mwenendo
wa biashara ya utalii nchini kwa kukusanya na kuainisha takwimu za
utalii wa ndani na wa kimataifa.
BODI YA UTALII TANZANIA
64.
Mheshimiwa Spika, Bodi itaanza kutekeleza Mkakati Mpya wa Miaka Mitano
wa Utangazaji Utalii Kimataifa mwaka 2012/13. Aidha, Bodi itaendelea
kuhamasisha uanzishwaji wa miradi ya utalii wa kiutamaduni kwa kutoa
elimu ya uhamasishaji katika vikundi mbalimbali katika mikoa ya Kusini,
Kanda ya Ziwa na Nyanda za juu Kusini. Vilevile, Bodi itaendelea
kutangaza utalii kupitia michezo, ambapo pamoja na matangazo katika Ligi
Kuu ya mpira wa miguu ya Uingereza, imeweka matangazo ya utalii katika
kiwanja cha mpira wa miguu wa Kimarekani na soka kinachomilikiwa na
Kampuni ya Seattle SeaHawks ya mjini Seattle nchini Marekani.
65.
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Utalii itakamilisha kazi ya kuunda
utambulisho (destination brand development) baada ya kukamilisha kazi za
awali za kutathmini jinsi Tanzania inavyoonekana machoni mwa wageni
(image investigation) na kutafuta utambulisho (brand identity) kama
hatua muhimu za kuunda utambulisho ambao utasaidia kuimarisha muonekano
wa Tanzania na kutangaza nchi yetu pamoja na vivutio vyake kikamilifu.
WAKALA WA CHUO CHA TAIFA CHA UTALII
66.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Chuo kitaendelea kutoa mafunzo
katika fani za ukarimu na utalii ambapo udahili unatarajiwa kuongezeka
kutoka wakurufunzi 229 hadi 315. Aidha, Chuo kitaanzisha mafunzo ya
jioni katika fani ya Upishi na kutoa huduma ya kutembeza watalii Dar es
Salaam kwa malipo. Natoa wito kwa wananchi kujiunga na chuo hiki ambacho
kinatoa elimu yenye ubora na uhakika ambao utawapatia ajira katika
sekta rasmi na isiyo rasmi.
SEKTA NDOGO YA MAMBO YA KALE
67.
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kufanyia marekebisho Sheria ya
Mambo ya Kale ya mwaka 1964 na marekebisho yake ya mwaka 1979. Vilevile,
itaanza ujenzi wa kituo cha kumbukumbu na taarifa kwenye kituo cha
Mapango ya Amboni, kujenga nyumba ya mtumishi katika kituo cha Oldupai
na kukarabati nyumba ya mtumishi Kaole na Magofu ya Kilwa Kisiwani.
Aidha, Mkakati wa utangazaji na uendelezaji wa vituo vya malikale
utaandaliwa pamoja na kuendeleza zoezi la kufukua na kuhifadhi nyayo za
binadamu wa kale zilizopo kwenye eneo la Laetoli.
SHIRIKA LA MAKUMBUSHO YA TAIFA TANZANIA
68.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Shirika litaendelea kuandaa na
kushiriki matamasha mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu
shughuli za makumbusho kupitia vyombo vya habari. Aidha, Shirika
litaandaa michoro ya ujenzi wa Makumbusho ya Falsafa ya Mwalimu J.K.
Nyerere ya Ujamaa na Kujitegemea itakayojengwa Chamwino, Dodoma.
URATIBU, UTAWALA NA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU
69.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13, Wizara itafanya mapitio ya Mpango
Mkakati (2010-2013) na kuandaa Mkutano wa kisera utakaoshirikisha wadau
mbalimbali. Aidha, Mpango wa Miradi ya Uwekezaji wa muda mrefu
unaoainisha maeneo ya uwekezaji katika sekta za maliasili, malikale na
utalii utaandaliwa.
70.
Mheshimiwa Spika, jitihada za kuongeza ukusanyaji maduhuli
zitaendelezwa kwa kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi na kuendesha
mafunzo kwa watumishi. Kazi zitakazofanyika kwa lengo la kuongeza
ukusanyaji maduhuli zimeainishwa katika aya ya 115 ya Kitabu cha Hotuba.
SENSA YA WATU NA MAKAZI
71.
Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu, Mwezi huu wa Agosti, 2012
Tanzania itaendesha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. Kwa Wizara yangu,
zoezi hili lina umuhimu wa kipekee kwa sababu changamoto nyingi
zinazoikabili sekta ya Maliasili (hususan Wanyamapori na Misitu);
zinatokana na shughuli za kibinadamu katika hifadhi kama vile kilimo,
ujenzi wa makazi na ufugaji nyuki. Idadi ya watu na kasi ya kuongezeka
kwao na jinsi wanavyojitawanya katika maeneo mbalimbali ya nchi ina
athari katika uhifadhi wa Maliasili pale ambapo uhifadhi endelevu
hautazingatiwa. Hivyo, uchambuzi wa taarifa zitakazotokana na zoezi hili
utatoa takwimu muhimu zitakazowezesha Wizara kuboresha sera na mikakati
mbalimbali inayosimamia na kutoa msaada pale inapobidi. Nawapongeza
wote waliohusika na maandalizi ya zoezi hili na tunatoa wito kwa wakazi
wote kujitokeza kuhesabiwa.
SHUKURANI
72.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati
Mheshimiwa Lazaro S. Nyalandu, Naibu Waziri na Mbunge wa Singida
Kaskazini, Bibi Maimuna K. Tarishi, Katibu Mkuu na Bibi Nuru H.M Millao,
Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi wa Idara, Wakuu wa Vitengo na Taasisi
kwa ushirikiano wao katika kuniwezesha kutekeleza jukumu la usimamizi wa
Wizara. Vilevile, napenda kuwashukuru watumishi wote wa Wizara na
Taasisi zake pamoja na wadau wa sekta kwa juhudi wanazoonyesha katika
utekelezaji wa kazi mbalimbali za Wizara. Aidha, nichukue nafasi hii
tena kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa James Daudi Lembeli (Mb) kwa
ushirikiano walionipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara yangu.
73.
Mheshimiwa Spika, Kwa namna ya pekee, napenda kuishukuru familia yangu
kwa upendo na uvumilivu wao katika kuniwezesha kutekeleza majukumu
yangu. Nawashukuru kwa dhati, wapigakura wangu wa Jimbo la Bukoba Mjini
kwa kuniamini na kunichagua kuwa mbunge wao, naahidi kuwa nitaendelea
kuwatumikia kwa uwezo wangu wote. Aidha, nawashukuru Katibu wangu,
Katibu Muhtasi na Dereva ambao wamenipa ushirikiano wa karibu katika
kutekeleza kazi zangu.
74.
Mheshimiwa Spika, Wizara imetekeleza majukumu yake kwa ushirikiano na
wadau wa maendeleo kutoka nchi na asasi mbalimbali za kitaifa na
kimataifa pamoja na sekta binafsi. Nichukue fursa hii kuwashukuru wote
na kutaja baadhi ya wadau kama ifuatavyo: Finland, Japan, Marekani,
Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Ujerumani, AFD, AWF, AWHF, DANIDA, Finnida,
FAO, FZS, GIZ, ICCROM, IUCN, Jumuiya ya nchi za Ulaya, KfW, NORAD, Sida,
SPIDER, SNV, UNDP, UNESCO USAID, UNWTO, World Bank, WMF na WWF.
I. HITIMISHO
75.
Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza hotuba yangu, naomba niwaombe
Watanzania kushiriki, kwa mara nyingine, katika shindano jipya la
maajabu saba ya asili. Shindano hili, ambalo linajulikana kama Seven
Natural Wonders linaendeshwa kupitia tovuti ya
http://sevennaturalwonders.org na linashindanisha vivutio vya kila bara
tofauti, ili kupata maajabu saba ya asili ya dunia katika kila bara.
Kati
ya vivutio 12 vinavyoshindanishwa katika Bara la Afrika, Tanzania ina
vivutio vitatu ambavyo ni Mlima Kilimanjaro, Kreta ya Ngorongoro na
Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Naomba
kuchukua fursa hii kuwahamasisha na kuwaomba Watanzania wote kuvipigia
kura vivutio vya Tanzania vilivyoingizwa katika shindano hili. Ninaamini
kwamba shindano hili linaweza kuwa fursa moja nzuri kwa Tanzania
kujitambulisha na kwa njia moja kuitangazia dunia kuwa Mlima
Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu kuliko yote barani Afrika; Hifadhi ya
Taifa Serengeti, ambapo tukio la kuhama wanyama hutokea kila mwaka; na
Kreta ya Ngorongoro, Kreta ya pekee duniani ambayo iko kamili na yenye
wanyamapori wa aina mbali mbali.
76.
Mheshimiwa Spika, ili Wizara iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka
2012/13, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi
77,249,692,390. Kati ya fedha hizo, Shilingi 26,665,371,000 ni kwa ajili
ya Mishahara, Shilingi 37,871,639,000 kwa Matumizi Mengineyo na
Shilingi 12,712,682,390 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.
77. Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa Hoja.