Utafutaji haramu wa Uranium, Zitto ataka kauli ya
Serikali.
Saadani National Park na Serengeti International
Airport zapigiwa chepuo.
MHE. KABWE Z. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nitumie dakika hizi chache
zilizobakia, kwanza napenda kuwapongeza wote upande wa Serikali na upande wa
Upinzani kwa hotuba zao na ninaomba Serikali iweze kuzingatia maoni ya Kambi ya
Upinzani na kuweza kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba ufafanuzi
nimeangalia ukurasa wa 60 wa Hotuba ya Bajeti kuhusiana na Halmashauri ambazo
zimepatiwa fedha za mgawo wa uwindaji asilimia 25, Halmashauri ya Wilaya ya
Kigoma haipo, na kuna mapori ya uwindaji. Huko nyuma tumekuwa tukipata mgawo
kidogo. Naomba nipate maelezo ni kwanini katika kitabu cha Waziri hakuna mgawo
huo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Utafutaji haramu wa Uranium unaofanywa na kampuni
ya Game Frontiers Ltd.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Wizara ya
Nishati na Madini, hotuba ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, na leo
katika hotuba ya Wizara ya Maliasilina Utalii ya Kambi ya Upinzani
tumezungumzia suala la mkataba wa kutafuta uranium kati ya kampuni ya Uranium Resources
na kampuni ya Game Frontiers Ltd ambayo kwa njia zote imekiuka sheria ya
madini ya mwaka 2010, sheria ya zamani ya madini ya mwaka 1997, Sheria ya
Wanyamapori, Sheria ya Ardhi, na mpaka sasa hatujapata kauli rasmi ya Serikali
kuhusiana na jambo hili. Tunaomba Serikali itoe kauli rasmi kuhusiana na
kampuni binafsi iliyopewa kibali cha uwindaji lakini ikaingia mikataba kwa
ajili ya utafutaji wa uranium.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni muhimu sana
liweze kuchukuliwa hatua ili kuweza kuzuia na kuweza kuona kama kuna maeneo
mengine ambapo jambo kama hili pia linafanyika. Naomba tuweze kupata kauli ya
Serikali kuhusiana na kampuni ya Game Frontiers na kampuni ya Uranium
Resources.
Tulenge Watalii milioni mbili
[MHE. KABWE Z. ZITTO]
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la Tatu; naomba
kuzungumzia kuhusu potential ya utalii. Tunafahamu kwamba utalii
ndiyo sekta ambayo inaingiza fedha za kigeni ya pili baada ya madini. Lakini
tofauti ya utalii na madini ni kwamba madini yanachimbwa yanapelekwa nje,
utalii watu wanakuja wanaangalia, wanaondoka. Kwa hiyo utalii unabakia. Kwa
hiyo hii ni resource ambayo inabakia. Kwa hiyo kuna kazi muhimu sana
ambayo ni lazima watu tuifanye kwa ajili ya kuhakikisha kwamba utalii unaongeza
fedha zaidi za kigeni. Mara kadhaa nimekuwa nikimwambia Waziri kwamba target
yetu ya watalii milioni moja pamoja na kwamba hatujaifikia, lakini bado ni
kidogo sana. Kwa potential tuliyonayo Tanzania, tunapaswa kuweka target
katika miaka mitano inayokuja ya kufikia watafikia watalii milioni mbili na
tunaweza tukaifikia iwapo tutarekebisha baadhi ya mambo fulani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi
imeonekana kwamba Taifa ambalo utalii unakua sana kwa watu wanaotoka ni Russia,
kwa hiyo ni lazima tujipange kama nchi, ikiwemo kuwa-train Watanzania
lugha yao. Kuna Watanzania ambao wanajua hivi sasa Kirusi lakini tuwaandae
vijana kwa ajili ya kuwa-train Kirusi kwa ajili ya kukuza utalii kutokea
Russia. Lakini China Vilevile, Korea na India hizi ni nchi ambazo sasa hivi
zinatoa watalii wengi sana. Kwa hiyo ni vizuri tuweze kujikita tuondoke katika
idadi ya watalii laki nane na elfu sitini na saba ambao tunawapata hivi sasa
tuende na target milioni mbili. Ninaamini kwamba tukifika huko tutakuwa
tumepunguza sana tatizo letu la balance of payment kwa sababu sasa hivi
mauzo yetu nje ni takribani dola bilioni sita tu, wakati manunuzi yetu nje ni
tarkibani dola bilioni 11. Kwa hiyo utalii unaweza kutusaidia kuweza kuweka
sawa urari wa kibiashara.
[MHE. KABWE Z. ZITTO]
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nina vitu viwili
ambavyo nilikuwa napenda tuvitilie nguvu zaidi Bodi ya Utalii; Bodi ya Utalii
inatangaza utalii nchi nzima. Kuna maeneo ambayo tuko disadvantage. Tuna
hifadhi, tuna vivutio lakini matangazo yake siyo makubwa. Katavi National
Park, Mahale National Park, Gombe National Park, na maeneo ya
kale kama Livingstone ya Ujiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri tuweze kuangalia
namna ambavyo mamlaka nyingine ziweze kufanya matangazo yao, kwa mfano TANAPA.
Hakuna sababu yeyote ya msingi kuwazuia TANAPA kuwa na Idara yao ya marketing
ili wauze product zao kama TANAPA, ili kuweza kukuza maeneo mengine
ambayo hatupati watalii kwa sababu tu ya matangazo na masuala mengine ya
kimiundombinu ambayo naamini kwamba Wizara zingine zitaweza kuyashughulikia.
Saadani NationalPark ipewe kipaumbele
kikubwa
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna eneo very unique
ambalo ni Saadani National Park. Ninapenda kuwashauri Wabunge wakipata
muda, Saadani ni karibu sana na Dar es Salaam waende Saadani National Park.
Hii ni hifadhi ambayo ikifanyiwa kazi vizuri Serengeti haitaona ndani. Kwa
sababu ni hifadhi pekee ambayo maji chumvi na maji baridi yanakutana na
yanakutana na bush. Bahari ya Hindi, mto Wami na hifadhi yenyewe ya
Saadani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba
tuifanyie matangazo maalum Sadaani. Saadani is very close to Dar Salaam,
Sadaan is very close to Zanzibar, Sadaani is very close to
Bagamoyo. Kwa hiyo, tunaweza tukaifanya Saadani kama project
inayojitegemea kwa ajili ya kukuza utalii. Lakini pili hata utalii wa ndani
tuweke utaratibu.
[MHE. KABWE Z. ZITTO]
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna reli inayopita Saadani
kwenda Tanga, tuongee na watu wa Wizara ya Uchukuzi kuwe na weekend trains
ambazo zinaenda Saadani kwa watu ambao wanataka kwenda over the weekends
na kuongeza idadi ya watalii ambao wanapita pale Saadani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tufanye project
maalum TANAPA na Wizara na Shirika la Reli kuhusu Saadani National Park.
Ni hifadhi ambayo inakumbukumbu za asili, ni hifadhi ambayo imejaa historia,
lakini pia ni hifadhi ambayo inaweza ikatuingizia mapato mengi sana ya kigeni.
Serengeti International Airport, Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni Mwanza.
Watu wengi sana wanadhani kwamba Arusha ndiyo njia ya kwenda Serengeti, Mwanza
ni karibu zaidi na Serengeti kuliko sehemu nyingine yeyote ukiachana na Wilaya
za karibu kama Serengeti na Bunda. Naomba tuwe na project maalum ya Airport
ya Mwanza, na kuna kampeni ambayo sasa hivi inaendelea ya airport ya
mwanza kuifanya kuwa ya Kimataifa na kuiita Serengeti International Airport.
Tufanye kampeni maalum tuhusishe wadau wote na Airport ya Mwanza kama
jinsi ambavyo tulivyojenga KIA kwa ajili ya utalii wa Kaskazini, tuijenge
Serengeti International Airport Mwanza kwa ajili ya utalii wa Kanda ya
Ziwa na utalii wa Magharibi ndege za kimataifa ziweze kutua, kwa ajili ya
kukuza eneo hili kiutalii. Serengeti ni karibu zaidi na Mwanza kuliko Arusha
ilivyo karibu na Mwanza.
[MHE. KABWE Z. ZITTO]
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba ni lazima
circuit ya Kaskazini kwa sababu ndiyo ambayo inatoa mapato mengi zaidi
kwenye utalii kwa hivi sasa ni lazima tuiendeleze kwa sababu yenyewe ndiyo
inatuzalishia fedha, lakini tutumie fedha hizo kukuza hayo maeneo mengine
ambayo yanaweza yakatusaidia. Kwa hiyo ninaomba kampeni hii ya Serengeti
International Airport Mwanza, iweze kukuzwa na tuweze kuiendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana ahsante
sana.
NAIBU SPIKA:
Waheshimiwa Wabunge, lakini kabla sijatoka hapa kwa
nusu sekunde na mimi niseme kidogo. Jirani zetu ambao tunashindana nao mara
nyingi wa Kenya, asilimia sitini ya utalii wao ni utalii wa Pwani ambapo ni
maeneo ya Mombasa Lamu na Malindi. Wanategemea Marine, National Parks na
Marine Reserves. Sisi Marine Reserves na National Parks
zetu tulizo nazo zipo chini ya Wizara ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Jana
tulikuwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni nani aliongelea habari ya Utalii jana?
Hivi ni kwanini Marine Parks na Reserves zisihamie Wizara ya
Maliasili na Utalii?
Kutamba kote kwa Kenya kunategemea Marine
Parks and Reserves na sisi tuna Marine Parks and Reserves bora
kabisa kuliko Kenya by far.
Kwa hiyo, naomba tupange mambo yetu vizuri,
tukiwakabidhi Marine Parks and Reserves, TANAPA au Wizara ya maliasili
na Utalii nina uhakika tunaweza tuka-double idadi ya watalii wetu kwa
haraka sana.