KANALI MASSAWE AHIMIZA VIJANA KUFUGA NYUKI

Na Renatha Kipaka, Bukoba WAKAZI wa mkoa wa Kagera, wameshauriwa kuanzisha ufugaji wa nhuki, ambao ni mradi rahisi usiohitaji fedha nyin... thumbnail 1 summary

Na Renatha Kipaka, Bukoba
WAKAZI wa mkoa wa Kagera, wameshauriwa kuanzisha ufugaji wa nhuki, ambao ni mradi rahisi usiohitaji fedha nyingi na unatoa faida kubwa kwa wafugaji.

Rai hiyo, imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe wakati akifunga maonyesho ya wakulima ya Nane Nane, yaliyofanyika mjini hapa.

Kanali Massawe, alisema asali ni zao lenye soko kubwa ndani na nje ya nchi, ambapo ndoo moja ya lita 20, inauzwa Sh 300,000.

Alisema kwa wastani, mkoa wa Kagera kwa mwaka mmoja unazalisha tani 180 za asali na tani 25 za nta.

Alisema hali ya uzalishaji wa asali bado iko chini, ikilinganishwa na fursa yenyewe ya ufugaji wa nyuki haijatumika ipasavyo, kwani mpaka sasa mkoa una mizinga ya nyuki 17,000, wafugaji 2,700 na vikundi 89 tu.

Alisema, asali inayozalishwa mkoani hapa, ina ubora na kiwango cha hali ya juu kuliko asali ya nchi yoyote duniani, kutokana na miti ya miombo inayopatikana katika hifadhi za misitu na mapori ya akiba.

Aliwasisitiza vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa, kujitokeza kwa wingi, kwa ajili ya kushiriki ufugaji wa nyuki.

Alisema hivi sasa soko la zao hilo, limepata ahueni baada ya kiwanda cha kusindika asali kuanzishwa mkoani Pwani.
Chanzo: Mtanzania