Na: Florence Majani,MWANANCHI
KWA
wakazi wa Dar es Salaam, mawingu yanapotanda angani na kutengeneza giza
ambalo huashiria mvua, kwao huwa ni jambo la kawaida na pengine ni
ahueni kwa karaha za joto kali. Lakini kwa wakazi wa mkoa wa Rukwa,
ikiwemo hasa Sumbawanga, dalili ya mvua inayoambatana na radi ni tishio
la umauti, kwani mara nyingi radi hizi si za kawaida au za asili bali ni
za kichawi na hutengenezwa na wanadamu kwa madhumuni ya kuua.
Mkoa
wa Rukwa hususani wilaya ya Sumbawanga, ni eneo linalosifika kwa imani
za kishirikina nchini. Lakini katika masuala ya utaalamu wa radi, yapo
maeneo na watu maalum ambao wana uwezo wa kutengeneza radi. Ukiwa
unatokea wilaya ya Sumbawanga kuelekea wilaya ya Nkasi, ndipo vilipo
vijiji maarufu kwa kutengeneza radi hizo.
Baadhi
ya vijiji hivyo ni Sintale na Chipu, ambako ndiko walipo wataalamu
wenye uwezo na nguvu za ziada za kutengeneza radi. Kwa nini radi
zinatengenezwa? Radi hizi zinatengenezwa kwa ajili ya kuua au kuwajeruhi
maadui. Kwa mfano, kama yupo aliyekudhulumu, aliyekuibia mke au mume,
aliyekugonga na gari bila kukulipia gharama za matibabu au anayekutusi
na kukukebehi. Vijiji vya Sintale, Chipu na Kalundi, vimepakana,
kinaanza kijiji cha Kalundi kisha Sintale na cha mwisho ni Chipu. Vijiji
hivyo viko duni kimaendeleo na ukubwa.
Hata
hivyo huku ndipo walipo watalaamu na mafundi wa kuunda radi.
Nilipokuwa mkoani humo hivi karibuni na mwenyeji wangu, tulielekezwa na
wenyeji wa Kalundi kwa mganga wa kwanza nayeitwa Mashaka ambaye
anaaminiwa kwa kuunda radi. Baada ya kufika kwa Mashaka, tunamkuta
akiwa na wateja kadhaa. Ninamweleza shida yangu na kumtonya kuwa ni
shida ya kipekee kidogo. Namweleza kuwa nahitaji kununua radi kwani
nina adui yangu aliyenidhulumu fedha nyingi. Mashaka anajibu kuwa yeye
si mtaalamu wa radi bali anatibu maradhi tu.
Anasema:
“Lakini yupo mtaalamu wa radi, anaitwa mzee Chimwaga, anaishi kijiji
cha Sintale. Ngoja nimpigie simu sasa hivi,” Mganga huyu anazungumza
kwenye simu kwa lugha ya kifipa, na baada ya dakika chache anakata simu
na kutugeukia na kusema: “Yupo- nendeni- kutoka hapa kwenda Sintale kwa
Honda ni dakika 20, mkimuuliza yeyote, atawapeleka kwa mzee huyo,” Kwa
kuhofia muda, hatukwenda kwa mganga Mzee Chimwaga, na badala yake
tunakwenda eneo jingine na kuuliza iwapo kuna mganga mwingine mwenye
utaalamu wa radi. Mzee mmoja anatuelekeza kuwa yupo mganga anayeitwa
Ntoro, mwenyeji wa hapo hapo Kalundi ambaye naye ni mtaalamu wa radi.
Tunaelekezwa
kwa mganga Ntoro, tunapofika tunamkuta akiwa na wake zake wawili na
watoto wasiopungua wanane. Anatukaribisha na tunamweleza shida yetu.
Mganga Ntoro anasema, yeye hutengeneza radi lakini kwa wakati ule
alikuwa kaishiwa vifaa, hivyo aliamua kumpigia simu mganga mwenzake
mwenyeji wa kijiji cha Sintale ambaye ana ujuzi huo pia.
Anashika
simu, na kumpigia mganga huyo tuliyebaini kuwa anaitwa Maisha, huku
akimsisitizia afike haraka azungumze na wateja. Wakati tukimsubiri
Mganga Maisha afike, tulianza kumdodosa Mganga Ntoro kuhusu utaalamu huo
wa kuunda radi. Ntoro anasema, kwa kawaida huduma ya radi huuzwa, au
hutozwa gharama kwa bei ya kuanzia Sh40,000 hadi 30,000 tu na hiyo ni
kulingana na umbali wa eneo alipo mtu anayetakiwa kuuwawa na aina ya
radi.
“Kwa
mfano watu wanaotoka Zambia au Kongo tunawachaji fedha nyingi zaidi kwa
sababu ya umbali, lakini kwa maeneo ya karibu bei ni nafuu kidogo,”
anasema Ntoro. Radi hutengenezwaje? Ntoro anasema, kwa kabila la
kifipa, utaalam wa kuunda radi huitwa ‘Namasata’. Radi hutengenezwa
kichawi, lakini mtu yeyote anaweza kufundishwa na kuweza kuitengeneza,
ili mradi afuate masharti. Anasema zipo radi za aina tatu, ya kwanza ni
ya maji, ya pili ni ya pembe, na ya tatu ni ya gome la mti. Zote hizo
hutengenezwa kulingana na umbali na ubora wake.
“Radi
ya pembe ni ya hatari zaidi, huchoma na kuweza kutekeza watu na mali,
na huenda umbali mrefu tofauti na radi ya gome la miti,” anasema Huku
tukiendelea kumdadisi, mganga Ntoro anasema, radi ya maji hutengenezwa
kwa kuchukua sahani mpya, bakuli mpya au chupa ya udongo. Kisha mtaalamu
huweka dawa ndani ya chupa au bakuli na kuisemea maneno fulani.
“Ukishanuiza,
unaviweka vifaa hivyo ndani, kesho asubuhi utakuta maji ndani ya chupa
au kama uliweka bakuli basi utaona maji ndani ya bakuli,” anasema na
kuongeza, “Baada ya hapo unachukua vifaa vile na kuanza kunuiza
adhabu unayotaka impate mbaya wako, kwa kumtaja jina. Kama huna jina
basi uwe na nyayo zake, nguo au kitu chake chochote kile.”
Anasema
baada ya kunuiza, unachukua bakuli au chupa ikiwa juu ya sahani na
kuyarusha maji yale juu, kwa nguvu za kichawi, maji yale hupotea lakini
kama kutakuwa na kasoro yeyote, maji yale humrudia aliyeyarusha. Endapo
mtaalamu atairusha radi ile kwa mtu asiye na makosa, basi maji yatarudi
chini na kama kweli mtu yule amefanya kosa, basi maji hayatarudi na
yatakwenda angani na kuanza kutengeneza wingu jeusi linaloambatana na
ngurumo.
“Maji
yakisharushwa juu, baada ya saa moja tu, utaanza kuona angani kiwingu
cheusi na kizito sana, mvua inaweza kunyesha kidogo na kisha ngurumo za
kutisha … basi hapo ujue kazi tayari na mbaya wako kashamalizwa,”
anasema na kuongeza: “Kama unairusha radi kwa mtu asiye na makosa
kabisa, au ukakosea masharti radi inaweza kukurudia na kukuunguza
wewe.
Mtu
akiniudhi mimi huwa nazirusha tu,” Radi ya pembe hutengenezwaje?
Wakati tukiendelea kumsubiri mganga Maisha, kutoka Chipu, Mganga Ntoro
anaendelea kutupa utaalamu huo bila kujua kuwa alikuwa akichunguzwa.
Sasa anasimulia namna ya kutengeneza radi ya pembe. Anasema, radi hii
hutengenezwa kwa pembe ya mbuzi au kondoo, ambayo kwa kawaida huwa na
uwazi katikati.
‘Tunachukua
pembe, tunaweka dawa ndani yake, (yaani kwenye uwazi) tunafunga hirizi
kuizunguka pembe, pamoja na shanga, kisha tunanuiza maneno kadhaa ya
kichawi, na kisha tunairusha kuelekea alipo mlengwa,” anasema Radi hii
ni kama kimondo, inaporushwa, hupaa angani na hufuka moshi katika upande
wa mbele wa pembe wenye uwazi kama zifanyavyo ndege za
kushambulia(rocket). Mganga Ntoro anasema, radi hii huweza kupaa
umbali mrefu na huweza kuharibu mali, mifugo na binadamu ambaye
anawindwa.
Kuhusu
namna ya kutengenez radi ya gome la mti, Ntoro anasema hiyo ina
masharti makali ambayo si rahisi kuzitoa siri zake kwa kila mtu. Hata
hivyo, baada ya muda mfupi, mganga Maisha anapiga simu na kusema kuwa
ameshindwa kufika kwa sababu ametingwa na shughuli za mazishi na kutaka
twende siku inayofuata asubuhi na mapema.
Mkazi
mwingine wa kijiji hicho, David Ntare anasema mauaji ya radi ni jambo
la muda mrefu mahali hapo kwani wanaotumia uchawi wa radi wamekuwa
wakijigamba mitaani kwa uweza wao huo. “Tangu nazaliwa nasikia vifo vya
radi na nina uhakika si radi za kawaida kwa sababu, wanaokufa mara
nyingi huwa na uhasama na mtu, kama kumuibia mke,mume, kuiba au
kutukana,” anasema Ntare.
Ntare
analihusisha tukio la kuungua kwa benki ya NMB, wilayani Nkasi, tarafa
ya Namanyere lililotokea miaka ya nyuma na uchawi wa radi. “Ile benki
iliunguzwa na radi na mzee mmoja mkulima wa kijiji cha Kizi baada ya
aliibiwa hela nyingi katika akaunti yake, akaona alipe kisasi kwa njia
ile. Ile benki iliungua wa radi, hakuna asiyejua,” anasema Inadaiwa
kuwa wenyeji wa hapa aghalabu huviona vitu hivi na hujua madhumuni yake
na mara nyingi vifo vya aina hii hutokea wilayani Sumbawanga. Anasema,
kwa kawaida mtu aliyeungua kwa radi huwa kama aliyeungua kwa umeme.
“Huungua
na kuwa weusi kama mkaa, na wakati mwingine radi hukataa kumuua mtu
akiwa ndani, bali humrusha nje na kumchoma huko ili isiwadhuru watu
wengine,” anasema. Mwalimu wa shule ya msingi Chalantala, Abeid
Kisanga, anasema siku moja akiwafundisha wanafunzi wa darasa la tatu
somo la sayansi kuhusu radi , mwanafunzi wa kiume alinyoosha kidole na
kusema ‘mimi najua kutengeneza radi, baba kanifundisha,”
Anjelo
Singo, Afisa wa Polisi tarafa ya Namanyere anasema suala la ushirikina
wilaya ya Sumbawanga na Nkasi ni kubwa na yamekuwapo matukio kadhaa ya
vifo vinavyodaiwa kusababishwa na imani hizo. “Ingawa serikali haiamini
uchawi, lakini matukio ya radi yanayotokea hapa mengi ni ya
kishirikina, au matukio ya watu kuuwawa na kukatwa sehemu za siri
vilevile ni ya kishirikina,” anasema Anasema ni ukweli usiopingika kuwa
uchawi umesheheni katika maeneo haya na wakazi wake wameshaathirika
kisaiolojia kuhusu hilo.
Mkuu
wa mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya anasema ameshawahi kusikia
taarifa za kuwepo kwa wataalamu wa kuunda radi lakini akasema hata hivyo
hana uhakika nazo. “Unajua jiografia ya mkoa wa Rukwa imekaa katika
nyanda za juu, ni rahisi radi kulipuka maeneo haya. Hata hivyo hili
suala ni la kiimani zaidi,” anasema pamoja na mambo mengi yanayosemwa
kuhusu mkoa huo, kwa sasa maendeleo yanakwenda kwa kasi na anaamini
miaka michache ijayo, imani za ushirikina zitapungua kama sio kwisha
kabisa.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz