WANANCHI, WANAJESHI WAPIGANA WAKIGOMBEA ARDHI

Na Rose Chapewa, Morogoro  VURUGU za kugombea maeneo kati ya wananchi wa Kijiji cha Chita na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JW... thumbnail 1 summary
Na Rose Chapewa, Morogoro 
VURUGU za kugombea maeneo kati ya wananchi wa Kijiji cha Chita na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zimeibuka, baada ya wananchi kuwavamia askari hao waliokuwa wakipima na kugawa maeneo katika eneo lenye mgogoro na kuanza kuwapiga kwa silaha za jadi.

Taarifa kutoka eneo la tukio zilidai kuwa awali askari takriban watano waliingia juzi saa sita mchana katika eneo la Kijiji cha Chita na kuanza kupima maeneo ya mashamba yanayogombewa baina ya JWTZ dhidi ya wananchi.


Hata hivyo, inadaiwa mmoja wa wananchi anayedaiwa kumiliki eneo hilo alipiga yowe za kuita wenzake ambao walifika eneo hilo na kuanza kuwavamia askari hao kwa silaha za jadi, lakini askari wengine walikimbia na kubaki mmoja aliyepigwa na kujeruhiwa na wananchi hao.

Inadaiwa askari waliokimbia waliwasiliana na wenzao walioko Kikosi cha 837 KJ na askari zaidi ya 50 walifika eneo hilo na kuanza kuwapiga wananchi waliowakuta kwa kutumia mabuti, mikanda, fimbo na virungu, huku wakifyatua risasi hewani kuwatawanya.

Mashuhuda wa tukio hilo walidai askari hao waliendelea kuzungukia maeneo hayo na kuchoma nyumba za wakazi na takribani nyumba tatu zilichomwa moto, mazao yaliyohifadhiwa yaliharibiwa, huku nyumba nyingine zaidi zikivunjwa na watu waliokutwa maeneo hayo walipigwa na askari hao.

Ilidaiwa kuwa wanajeshi hao walivamia hadi katika eneo la Mikumi lenye maeneo ya biashara na kuanza kuvunja mabanda ya biashara na kunywa soda zilizokutwa katika maeneo hayo.

Baadhi ya watu, wakiwamo Gozianus Ngwada, Natalia Miyonjo, Mbaga Masanja, Musa Singu, Francis Msita, James Chilimba, Venance Lupumbwe, Castory Mwagala na Tryphone Mkumba walijeruhiwa na kupelekwa kupata matibabu katika zahanati ya kijiji hicho.

Wananchi waliojeruhiwa wamepata zaidi majeraha sehemu za kiuno, kichwani na maeneo mengine ya mwilini.

Aidha, askari mmoja wa kikosi hicho aliyevamiwa na wananchi alikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya St Francis iliyopo Ifakara na amelazwa wodi namba mbili kwa ajili ya matibabu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hassan Masala, alikiri kutokea kwa vurugu hizo zilizosababishwa na wananchi kuwazuia askari kupima maeneo.

Hata hivyo, alisema tayari Jeshi la Polisi limewatia nguvuni baadhi ya watu wanaodaiwa kuanzisha vurugu hizo na wanasubiri taratibu zaidi za kisheria kuchukua mkondo wake.
Chanzo: Mtanzania