BALOZI KAGASHEKI AZIONYA NGO's ZA ULAYA, AZITAKA KUACHA KUIPANGIA TANZANIA KUUZA PEMBE ZA NDOVU

Na Eliya Mbonea, Arusha  WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Hamis Kagasheki, ameyashukia na kuyaonya Mashirika yasiyokuwa ya Serikali (... thumbnail 1 summary

Na Eliya Mbonea, Arusha 

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Hamis Kagasheki, ameyashukia na kuyaonya Mashirika yasiyokuwa ya Serikali (NGO’s) na wanaharakati wa Ulaya kuacha kuipangia Tanzania kuhusu uamuzi wa kuuza pembe za ndovu.

Mbali na onyo hilo, aliziambia kuwa Tanzania iko tayari kuteketeza pembe za ndovu endapo NGO’s hizo zitakuwa tayari kutoa mabilioni ya fedha.


Akizungumza mjini hapa juzi, Balozi Kagasheki, alisema NGO’s na Wanaharakati hao hawana haki ya kuipangia Tanzania uamuzi wake wa kuuza meno ya ndovu, kwa kuwa uamuzi huo unalenga kupata fedha kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo.


“Mvutano wa kuuza au kuteketeza meno ya tembo yaliyohifadhiwa si wetu tu, Zambia, Afrika Kusini na Namibia wapo kwenye mvutano huu nao wanataka kuuza meno waliyohifadhi.

“Hizi NGO’s zinapinga uamuzi wetu wanataka tuziteketeze kwa moto, Tanzania tunasema kama wapo tayari kutulipa tuziteketeze walete fedha,” alisema Balozi Kagasheki.

Hata hivyo, alisema suala hilo linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano utakaofanyika nchini Thailand mwaka 2013.

Alisema Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti biashara ya kimataifa wa wanyama na mimea iliyo hatarini kutoweka (Cites), uliosainiwa mwaka 1973 na kuanza kutekelezwa mwaka 1975, huku Tanzania ikiuridhia mwaka 1980.

Alisema mwaka 1988, Tanzania ilisimamisha biashara ya meno ya tembo, hatua iliyoonyesha nchi kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za Cites.

Katika muswada wake kwa Sekretariet ya Cites wa kuuza meno ya Tembo, Tanzania iliwasilisha maombi ya kuuza kilogramu 90,000 ambazo zingeweza kuingiza kiasi cha Dola milioni 20 za Marekani.
Chanzo: Mtanzania