Na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam.
KATA tatu za Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, zinaongoza kwa
uchafu. Kutokana na hali hiyo, inawalazimu wasimamizi wa sekta ya afya,
kuanzisha kampeni endelevu ya usafi ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.
Akizungumza jana wakati wa kampeni endelevu ya usafi katika Kata ya
Ilala ,Ofisa Afya, Idara ya Usafirishaji Manispaa ya Ilala, Charles
Wambura, alisema kata hizo huzalisha tani 170 kwa siku.
Alizitija
kata hizo kuwa ni Buguruni, Ilala na Vingunguti na kwamba, kwa sasa
kuna mikakati iliyowekwa ili kutokomeza uchafu katika kata hizo.
Katika
Kata ya Ilala, alisema wananchi huzalisha tani 35 kwa siku, Vingunguti
tani 60 na Buguruni tani 75 hadi 80, huzalishwa kwa kuwa katika kata
hiyo kuna soko kubwa.
"Tumeanza kuweka kambi katika kata hizo, kwa ajili ya kampeni endelevu ya usafi, ili kuepuka magonjwa ya milipuko.
“Lakini
pia tumekumbana na changamoto mbalimbali, ikiwamo wananchi kushindwa
kujitokeza katika usafi na kutokulipa ushuru wa taka," alisema Wambura.
Kwa
upande wake, Ofisa Afya, Kata ya Ilala, Azizi Mkote, alisema
wafanyabiashara 100 wa vipuri vya magari wameazimia kufanya usafi kila
Ijumaa na Jumamosi, ili kuhamasisha suala la usafi wa mazingira.
Naye,
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime, alisema manispaa hiyo
imesaini mkataba na wataalamu wa Serikali ya Ujerumani, ili kufanikisha
ujenzi wa kituo cha kuchambua taka kinachojengwa eneo la Gongo la Mboto.
Fuime
alisema kwamba, wametiliana saini mkataba huo na Kampuni ya Bremen
Overseas Research and Development Associations (BORDA) na kazi rasmi ya
kuchambua taka, itaanza Desemba mwaka huu baada ya ujenzi kukamilika.
Aliongeza kwamba, ujenzi wa kituo hicho ni mwendelezo wa kujenga vituo, kikiwamo kituo cha kuchambua taka kilichopo Vingunguti.
"Vituo
hivi vitakuwa vinachambua taka, baada ya kukusanywa na wananchi. Lengo
la kufanya hivyo kutaka taka zifikie zinakotakiwa kwenda zikiwa
malighafi,” alisema Fuime.
Chanzo: Mtanzania