Watanzania, viongozi watakiwa kutunza mazingira

Na Mwandishi Wetu, Mpanda. MWENYEKITI wa Shirika la Habari Njema kwa Wote, Askofu Charles Gadi, amewaomba Watanzania na viongozi kubadilik... thumbnail 1 summary
Na Mwandishi Wetu, Mpanda.
MWENYEKITI wa Shirika la Habari Njema kwa Wote, Askofu Charles Gadi, amewaomba Watanzania na viongozi kubadilika kimawazo, kitabia na kimatendo, katika kutunza mazingira, kwa ajili ya kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na uharibifu wa mazingira na ukame.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa katika maombi maalumu yaliyofanyika katika Mbuga ya Wanyama ya Katavi, ambako viboko wameanza kufa kutokana na ukame.


Akitolea mfano wa viboko wanaotaabika na wengine kufa kutokana na ukame, uliodumu kwa takriban miezi sita sasa, katika Mto Katuma uliomo katika mbuga hiyo, Askofu Gadi, alisema kama mazingira ya chanzo cha mto huo yangetunzwa vyema, wanyama hao wasingetaabika kiasi cha kufa.

Alisema wakazi wa Katavi na Watanzania kwa ujumla, wanapaswa kumcha Mungu, kwa kuwa hiyo ndiyo nguzo kuu ya kujitoa kwa moyo wote katika kutunza mazingira na wanyama waliomo.

“Binadamu ameacha kufanya mambo yanayompendeza Mungu, ndiyo maana haya yote yanatokea, wakati umefika kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua kunusuru maisha ya viumbe hawa wasiyo na hatia,” alisema Askofu Gadi.

Kwa upande wake, Mhifadhi Utalii, Costansia Maffa, alisema ukame unaondelea hivi sasa katika mbuga hiyo umeathiri maisha ya wanyama wakiwamo viboko na kuulazimu uongozi wa mbuga hiyo, kutumia njia mbadala za kuongeza maji kwa kutumia mipira inayopita chini kwa chini katika Mto Katuma.

“Binadamu hudhani kuwa wanyama ni adui, kumbe wanaweza kuwa msaada mkubwa sana kwao, iwapo watapata ushirikiano na mazingira yao, kutunzwa vizuri.

“Kutokana na ukame huu, maisha ya viumbe hawa kwa sasa yanategemea maombi yetu sisi sote, kwa sababu hawa kama wanyama hawawezi kupiga magoti na kumwomba msaada wa Mwenyezi Mungu, bali hilo ni jukumu letu binadamu,” alisema Maffa.

Naye, Katibu wa Huduma wa Shirika hilo, Mchungaji Palemo Massawe, aliwataka wahifadhi wa mbuga zote Tanzania kujiepusha na vitendo vya kushirikiana na majangili kwa sababu kufanya hivyo ni kulihujumu maendeleo ya Taifa.

“Hivi karibuni tumekuwa tukisikia kutoka katika vyombo vya habari kuwa baadhi yenu mnashirikiana na majangili kuwinda hawa wanyama, hii ni kinyume cha maadili ya kazi na mafundisho ya Mungu,” alisema Mchungaji Massawe.

Awali akifungua maombi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk. Rajabu Rutengwe, aliyataka mashirika ya dini kuuombea mkoa huo mpya na rasilimali zilizomo uweze kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Alisema hivi sasa mkoa huo unakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwamo za kijamii, afya, elimu na miundombinu ya barabara na Serikali inajitahidi kuzitafutia ufumbuzi.

“Nawashukuru waandaji wa mkutano huu. Maombi haya yatasaidia kuleta Baraka ya Mungu na hatimaye mkoa wetu mpya, upige hatua kubwa za kimaendeleo kwa haraka,” alisema Dk. Rutengwe.

Aidha, aliyataka mashirika mengine kuiga mfano wa huduma njema kwa wote na kuongeza kuwa, kila mtu kwa nafasi yake ni mdau wa maendeleo ya nchi.


Chanzo: Mtanzania