‘Katiba mpya ilinde rasilimali’

UGUMU wa maisha na kipato duni miongoni mwa wananchi vimeifanya  hoja ya rasilimali za taifa kama vile madini, gesi, misitu na wanyama kuwan... thumbnail 1 summary
UGUMU wa maisha na kipato duni miongoni mwa wananchi vimeifanya  hoja ya rasilimali za taifa kama vile madini, gesi, misitu na wanyama kuwanufaisha wananchi badala ya wageni kuendelea kupendekezwa ili iingizwe kwenye Katiba Mpya ijayo.

Pendekezo hilo lilitolewa na wakazi wa Ilala mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wananchi hao waliimbia Tume kuwa hakuna sababu ya Watanzania kuendelea kuwa masikini wakati nchi ina rasilimali za kutosha.


Walisema kuwa kinachotakiwa hivi sasa ni kuhakikisha Katiba ijayo inazisimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya wananchi wote bila kujali maeneo ambako rasilimali zinapatikana.
Muhidin Rashid (44) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa kata ya Jangwani alisema kuwa Tanzania ina madini na gesi ya kutosha lakani haziwanufaishi wananchi kama inavyotakiwa.
Ili kuhakikisha kuwa Serikali inazisimamia rasilimali hizo kwa manufaa ya wananchi, amependekeza Katiba Mpya ije na sheria itakayotamka na kutambua kwamba rasilimali ni mali ya wananchi na siyo vinginevyo.


“Napendekeza kuwa rasilimali zote zisimamiwe na Serikali kwa manufaa ya wananchi. Utaratibu huu utaiwezesha Serikali kutoa huduma za afya, elimu, umeme na usafiri kwa wananchi wake bila kutegemea wahisani au makampuni ya watu binafsi. Kutoa huduma kwa wananchi ni jukumu la Serikali kwa kutumia rasilimali zilizopo,” alisema Hadji Juma mkazi wa Kata ya Jangwani.


Mbali na hoja hiyo ya rasilimali, wananchi hao pia wamependekeza kuwa Katiba Mpya izuie marais na mawaziri wakuu wastaafu kuendelea kuhudumiwa na Serikali kwa maisha yao yote.


Wamesema kuwa kila baada ya miaka kumi kunakuwa na rais na waziri mkuu mstaafu hali ambayo ni mzigo kuwatunza kama ilivyo sasa ikizingatiwa kuwa idadi yao inazidi kuongezeka.


“Ni mzigo sana kwa Serikali kuendelea kuwahudumia viongozi hao wastaafu. Napendekeza Katiba Mpya itamke kuwa hakuna rais wala waziri mkuu mstaafu ataendelea kuhudumiwa na Serikali akishalipwa mafao yake,” alisema Hamisi Mashoto mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.


Pia wakazi hao wa Jangwani wamependekeza haki za binadamu hasa haki ya kuishi iendelee kulindwa kikatiba. Wameiambia Tume kuwa adhabu ya kifo iendelee kuwepo ili kutenda haki kwa aliyeuawa.  


John Ndunguru (43) alisema kuwa asasi za kiraia zinazopinga adhabu hiyo hazisemi lolote kuhusu stahili za aliyeuawa ili kutenda haki kwa pande zote mbili.


“Anayeua naye auawe ili haki itendeke. Kumekuwa na mauaji makubwa ya walemavu wa ngozi (Albino). Kesi zikifika mahakamani haziendi vizuri kwa hiyo dawa yake ni kuwanyonga tu wauaji,” alisema Abukar Ramesh

Chanzo: Mwananchi