Jangili aua polisi, nao wamuua kwa risasi

Watu wawili akiwamo askari polisi wamekufa mkoani Singida katika tukio la kurushiana risasi na kundi la majangili katika Kitongoji cha Ki... thumbnail 1 summary
Watu wawili akiwamo askari polisi wamekufa mkoani Singida katika tukio la kurushiana risasi na kundi la majangili katika Kitongoji cha Kirumbi, kilichoko katika Kijiji cha Kintanula wilayani Manyoni.
Kundi hilo la majangili, linatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya biashara haramu ya nyara za Serikali. Tukio hilo lilitokea Oktoba 31 mwaka huu katika operesheni kutokomeza ujangili inayoendelea wilayani Manyoni.
Askari aliyeuawa katika tukio hilo ametajwa kuwa ni mwenye namba G.9934 D/C Mgaka (26) wakati jangili ametambulika kuwa ni Selemani Kimpinde, mkazi wa kijiji hicho.
Akithibitisha tukio hilo baada ya kutembelea chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Mkuu wa wilaya hiyo, Fatma Taofiq, alisema baada ya askari huyo kumkamata jangili Seleman, walipanda gari na kuanza safari ya kwenda kuonyeshwa zilipo silaha aina ya SMG.
Alisema lakini walitembea umbali wa mita 100, kabla ya kufika kwenye eneo husika, askari hao waliamua kushuka kwenye gari na kuanza kutembea kwa miguu.
Taofiq alisema baada ya kufika kwenye eneo ambalo walitarajia kuonyeshwa silaha, alitokea jangili mwingine aliyekwenda kumpora askari silaha aliyokuwanayo.
“Wakati wa purukushani kati ya askari na jangili hilo lililomnyang’anya silaha, walijitokeza majangili wengine wawili na kumpiga risasi askari huyo. Baada ya askari kuanguka chini akiugulia maumivu, jangili huyo alianza kutimua mbio,” alisema.
Alisema jangili alikuwa hajawaona askari wengine waliokuwa wamejificha nje na kwamba waliposikia mlio wa risasi, askari aliyekuwa nyuma ya majangili hao alimpiga risasi jangili Kimpinde na kufa papohapo.
Chanzo: Mwananchi