Harakati za akina Mandela katika ardhi ya Tanzania

Katika  toleo lililopita  la gazeti hili, tulieleza mwenendo wa harakati za African National Congress (ANC) kupinga ubaguzi wa rangi ... thumbnail 1 summary




Katika toleo lililopita la gazeti hili, tulieleza mwenendo wa harakati za African National Congress (ANC) kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na namna Mwalimu Julius Nyerere alipokataa wito wa Mandela kuanzisha kambi za wapiganaji lakini baadaye kukubaliana na wito huo, baada ya kazi kubwa ya kumshawishi. Tunaendelea na sehemu ya mwisho ya makala hii, kama ilivyoandaliwa na mwandishi wetu.
MWAKA 1976, baada ya kutokea mauaji makubwa ya wanafunzi katika mji wa Soweto, yaliyotekelezwa na polisi wa makaburu, na hivyo kusababisha vijana wengi wa ANC kuikimbia Afrika Kusini na kwenda kuwa wakimbizi nje, chama hicho kiliona haja ya kuwa na shule yake nchini Tanzania ambayo ingetumiwa na vijana hao wa ANC waliokuwa wamekimbia kukwepa vipigo vya polisi.
Kutokana na hali hiyo, mwaka huo, ujumbe wa ANC uliwasilisha ombi kwa Mwalimu la kupatiwa ardhi ya kutosha ya kuweza kujenga shule zake, kuanzia chekechea, msingi na sekondari. Mwalimu alikubali ombi hilo la ANC na kuwakabidhi wajumbe hao kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wa wakati huo, Anna Abdallah ili awatafutie ardhi ndani ya mkoa wake.
RC Anna Abdallah, aliwachukua viongozi hao wa ANC, akiwamo Tambo hadi katika shamba la mkonge la Mazimbu na kuwakabidhi eneo hilo kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Elimu cha ANC (ANC Education Facilities). Mwaka 1978 ilizinduliwa rasmi shule ya kwanza ya msingi ya ANC Mazimbu, mwalimu wake mkuu akiwa Wintshi Njobe.
Mwaka 1979, ANC ilipata pigo kubwa baada ya mwanaharakati wake kijana, mwanafunzi bado wa shule, ambaye alikuwa mwiba kwa serikali ya kibaguzi ya makaburu, Solomon Mahlangu, kunyongwa hadi kufa baada ya Mahakama ya nchi hiyo kumtia hatiana na kutoa hukumu ya kunyongwa mwaka 1977, kwa madai ya kuendesha vitendo vya kigaidi.
Inasimuliwa kwamba wakati wa kutekeleza hukumu hiyo ya kunyongwa, Aprili 6, mwaka 1979, akiwa katika Gereza Kuu la Pretoria, makaburu walimwita mama yake na ndugu yake ili kushuhudia tukio hilo la kinyama.
Wakati Solomon akipandishwa kwenye kitanzi, kijana aliyekuwa amehitimu mafunzo ya Umkhonto wa Sizwe katika kambi za jeshi za ANC nchini Angola na Msumbiji kutokana na kukatishiwa masomo yake na Makaburu akiwa darasa la nane mwaka 1976, mama yake alianza kububujikwa machozi, lakini Solomon akamwambia mama yake kwamba hakuwa na sababu yoyote ya kulia, na badala yake akamwambia mama yake maneno yafuatayo:
“Tell my people that I love them and that they must continue the struggle, my blood will nourish the tree that will bear the fruits of freedom. Aluta Continue.” (Mama ninakufa, waambie watu wangu (Wana-ANC) kwamba nawapenda na waendeleze mapambano haya, damu yangu hii itakayomwagika ndiyo itakuwa kirutubisho cha mti ambao hatimaye utatoa matunda ya uhuru. Mapambano yanaendelea).
Baada ya tukio hilo la kunyongwa kwa mwanafunzi Solomon aliyekuwa na miaka 23, kituo cha elimu cha ANC Mazimbu, Morogoro, kilibadilisha jina la kituo hicho kama hatua ya kumuenzi mwanaharakati huyo, na kukiita Solomon Mahlangu Freedom College (Somafco) hadi mwaka 1992 kilipofungwa baada ya utawala wa makaburu kusalimu amri dhidi ya harakati za ANC, kwa kumwachia huru Mandela kutoka kifungo cha maisha, kuruhusu shughuli za kisiasa, kisheria na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, na hivyo kutimia kwa ndoto ya Solomon Mahlangu.
Solomon Mahlangu Campus, SUA
Kwa sasa eneo hilo la Somafco Mazimbu, linamilikiwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), baada ya Serikali kulikabidhi rasmi kwa chuo hicho mwaka 1998. Uongozi wa SUA kutokana na kuenzi mchango wa kijana Solomon katika harakati za ANC kusaka ukombozi wa Afrika Kusini, umebadili jina lake kutoka Solomon Mahlangu Freedom College na kuwa Solomon Mahlangu Campus (SMC).

Magdalena John, ni Ofisa Utawala wa kampasi hiyo ya SUA. Katika mazungumzo na Raia Mwema chuoni hapo hivi karibuni, anasema kituo hicho cha elimu cha ANC Mazimbu, mbali na kutoa elimu ya awali hadi sekondari, wanafunzi na wanaharakati wa ANC walikuwa wanajishughulisha pia na miradi mbalimbali ya kiuchumi ili kukiongezea uwezo wa kiuchumi kituo hicho.
Anaitaja baadhi ya miradi ya kijamii na kiuchumi iliyokuwa ikiendeshwa katika eneo hilo na wapiganaji hao wa ANC kuwa ni pamoja na hospitali iliyokuwa na hadhi ya mkoa ya daraja la pili, iliyokuwa ikiitwa kwa jina la ANC Holland Solidarity Hospital iliyozinduliwa rasmi Mei 4, 1984, na Oliver Tambo ambaye ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa ANC aliyekuwa akiishi mahali hapo hadi kinafungwa mwaka 1992.
Ofisa Utawala huyo anaitaja miradi ya kiuchumi kuwa ni pamoja ranchi ya mifugo iliyokuwa imesheheni ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku. Aidha, kulikuwa na mradi wa kiwanda cha ushonaji nguo na kiwanda cha kutengeneza samani (furniture) kilichokuwa kikijulikana kwa jina la Vuyisile Mini Furniture.
Kwa mujibu wa Magdalena, kutokana na ongezeko la wana ANC katika eneo hilo na pia kupanuka kwa mahitaji kwa jamii hiyo ya wana ANC, mwaka 1988/89 uamuzi ulifikiwa wa kukihamisha kiwanda hicho cha ushonaji wa nguo, ambazo nyingi ya hizo zilikuwa nguo za kivita kwa ajili ya wanapiganaji wa Umkhonto, na kukipeleka Dakawa ambako ANC ilikuwa imeanzisha kambi nyingine ya kutolea mafunzo ya kijeshi kama ilivyokuwa kwa Kongwa.
Kiwanda hicho cha nguo cha Dakawa, kilijulikana kwa jina la ANC Dakawa Arts & Craft. Mitambo ya kiwanda hicho pamoja na wafanyakazi wake wote vilihamishwa na ANC mwaka 1993 na kupelekwa Grahamstown, na hadi sasa shughuli hiyo ya ushonaji inaendelea chini ya jina hilo hilo la ANC Dakawa Arts & Crafts.
Wapiganaji hao wa ANC waliacha nini hapo Mazimbu? Yapo makaburi 97, kati ya makaburi hayo mawili yakiwa yamefukuliwa na wenye nayo na kuhama nayo kwenda Afrika kusini, yanayotokana na vifo vya watoto na watu wazima katika familia za wapiganaji wa chama hicho waliokuwa wakiishi hapo.
Lipo jengo moja karibu na makaburi hayo lililokuwa likitumika kama nyumba ya ibada, jingo kubwa la kiutawala na nyumba 162 za familia ambazo kwa sasa zinatumiwa na wafanyakazi wa kampasi hiyo ya SUA, madarasa 28, kumbi nne za mihadhara ya kitaaluma na ukumbi wa bwalo unaojulikana kwa jina la The Nelson Mandela Freedom Square.
Ipo pia mitaa kadhaa inayobeba majina ya miji ya mataifa ya nje, kama vile Copenhagen ili kuenzi michango ya hali na mali wa mataifa hayo, ikiwamo Denmark, katika harakati za ANC kutafuta ukombozi wa Afrika kusini, pamoja na mtaa wa Heroes (Mashujaa) unaoelekea kwenye makaburi ya mashujaa hao 97 waliozikwa katika makaburi hayo.
Nihitimishe makala haya kwa kusema juhudi za Mandela zinamwongeza mwanamapinduzi huyo katika orodha ndefu ya mashujaa wa taifa hilo la Afrika Kusini. Katika orodha hiyo, Govan Mbeki, Oliver Tambo, Solomon Mahlangu, Steven Biko, Chris Hani, Joe Slovo, Yusuf Dadoo, Walter Sisulu, Fatima Meer, Ashley Kriel, Anton Fransch, Joe Modise, Lilian Ngoyi, Tsietsi Mashirini, Helen Joseph, Ben Turok, Ambrose Makiwane, Miriam Makeba, Adelaide Tambo na wengine wengi wataendelea kuenziwa na kizazi cha sasa na kijacho cha ANC. 
chanzo: raia mwema