Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii (TTB)
imeandaa Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii yatakayokuwa yakifanyika kila
mwaka kuanzia mwaka huu.
Akizindua tovuti ya maonyesho hayo yanayotarajiwa
kuanza Oktoba 1-4 mwaka huu jijini hapa, Waziri Lazaro Nyalandu alisema
Serikali imejipanga kuhakikisha sekta hiyo inawanufaisha wananchi zaidi.
“Nitahakikisha tunawaalika mawaziri na mawakala wa
utaliikutoka nchi mbalimbali washirika wetu duniani. Tunatarajia
maonyesho haya yawe makubwa na yaitangaze Tanzania kama kituo muhimu cha
utalii duniani,” alisema Nyalandu.
Maonyesho hayo yatakayojulikana kama Swahili
International Tourism Expo (Site), yanatarajiwa kupanua wigo wa utalii
nchini hasa kwa kuvitangaza vivutio vya maeneo mengine ya nchi, hasa
kusini baada ya upande wa kaskazini kufanya vizuri.