CORAL BEACH HOTELI YAONDOA KIFUSI UFUKWENI

Na mwandishi wetu Uongozi wa Hoteli ya Coral Beach umetekeleza agizo walilopewa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa... thumbnail 1 summary
Na mwandishi wetu
Uongozi wa Hoteli ya Coral Beach umetekeleza agizo walilopewa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kuondoa kifusi chote ilichokilundika pembezoni wa ufukwe wa hoteli hiyo.

NIPASHE iliyotembelea hotelini hapo jana jijini Dar es Salaam ilishuhudia eneo hilo likiwa katika hali ya kawaida huku eneo hilo likiwa na mchanga wa kawaida unaozoeleka kuonekana pembezomi mwa bahari

Akizungumza kwa njia ya simu, Mwanasheria wa NEMC, Heche Machali Suguto, alisema kuwa kwa sasa yupo nje ya Dar es Salaam kikazi, lakini taarifa alizonazo ni kuwa uongozi wa hoteli hiyo umetii agizo alilolitoa hivi karibuni kwa kutoa kifusi hicho.

Suguto aliongeza kuwa suala la faini ambalo lilikuwa linakwenda sambamba na utoaji wa kifusi hicho, atalizungumzia atakaporudi jijini Dar es Salaam, baada ya kujiridhisha na kutekelezwa kwa amri aliyoitoa kwa kutembelea eneo la tukio.

Alisema  endapo mtu yeyote akipewa adhabu ya faini na maelekezo mengine, anaweza kufutiwa adhabu ya faini kama atatii na kutekeleza maelekezo aliyopewa.

Hivi karibuni, NEMC ilimuamuru hoteli hiyo kulipa faini ya Sh. milioni 10 pamoja na kuutaka ukiondoe kifusi katika kipindi cha siku saba, ilichokilundika pembezoni mwa ufukwe wa hoteli hiyo kwa lengo la kudhibiti mmomonyoko wa ardhi unaosababishwa na mawimbi ya bahari.
CHANZO: NIPASHE