MNYIKA ASEMA WIZARA YA NISHATI NA MADINI INAKUMBATIA UFISADI NA KUKWAZA UTETEZI WA RASILIMALI ZA TAIFA

Mbunge wa Ubungo(CHADEMA)John Mnyika --- Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo afute taarifa iliyotolewa na Katibu ... thumbnail 1 summary

Mbunge wa Ubungo(CHADEMA)John Mnyika
---
Waziri
wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo afute taarifa iliyotolewa na Katibu
Mkuu wa wizara hiyo kuwa lengo la agizo lake la kupitiwa kwa mikataba yote 26
ya utafutaji mafuta na gesi asili ni “kuhakikisha kwamba endapo kuna mapungufu
katika mikataba hiyo, mapungufu hayo yasijirudie tena katika mikataba mipya ya
baadaye” kwa kuwa ikiachwa ilivyo italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa
rasilimali za taifa.

Ufafanuzi
uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini unatoa mwanya kwa
mikataba mibovu kulindwa wakati ambapo kuna madai tuliyotoa toka mwaka 2011
kwamba baadhi ya mikataba hiyo imeingiwa kifisadi na mwaka huu wa 2012
zimeibuka tuhuma za vigogo wa serikali kuingiziwa fedha kifisadi katika akaunti
zao za nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji mafuta na gesi asili.

Tafsiri
ya ufafanuzi huo uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ni
kwamba hata kama mikataba iliyopo ina mapungufu yasiyozingatia maslahi ya
taifa, matokeo ya mapitio hayo hayatarekebisha mikataba iliyopo bali mikataba
ya baadaye.

Taarifa
hiyo ya Katibu Mkuu wa Wizara ni ya kurudi nyuma tofauti na kauli za awali za
Waziri Muhongo zilizokubaliana na madai yetu ya toka mwaka 2011 ndani na nje ya
bunge ikiwemo kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ya kutaka
mikataba yote ipitiwe upya, isiyozingatia maslahi ya taifa ivunjwe au ifanyiwe
marekebisho makubwa na mikataba mipya isiingiwe mpaka kwanza kuwepo sera na
sheria bora zenye kulinda uchumi na usalama wa nchi.

Itakumbukwa
kwamba tarehe 15 Septemba 2012 wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi
ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) Waziri wa Nishati na Madini
aliagiza bodi hiyo kuipitia mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili
ili kujiridhisha endapo maslahi ya taifa yalizingatiwa.

Agizo hilo
la Waziri limeendana na mapendekezo niliyotoa mwaka 2011 ya kutaka mapitio ya
mikataba yote ya mafuta na gesi asili ambapo pamoja na mambo mengine niliitaka
Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake kuacha kuingia
mikataba ya muda mrefu  ya utafutaji wa
mafuta na gesi asili katika maeneo mbalimbali nchini yenye mianya ya kuhujumu
uchumi wa nchi na haki za wananchi masuala ambayo yalipingwa na Waziri wa
zamani.
Kutokana na
kutozingatiwa kwa mapendekezo hayo tarehe 21 Februari 2012 nilitoa kauli ya kutaka
Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo William Ngeleja kuwajibishwa kwa
kuendelea kuruhusu kusainiwa kwa mikataba bila maagizo ya msingi kuzingatiwa na
kueleza kwa umma sababu za serikali kuendeleza usiri na kuacha kufanya mapitio
ya mikataba mibovu iliyopo.
Nilitoa
kauli hiyo baada ya tarehe 20 Februari 2012 Serikali kusaini mkataba wa
kutafuta mafuta na gesi asili na kampuni ya Swala katika maeneo ya Kilosa
Mkoani Morogoro na Pangani Mkoani Tanga na Januari 2012 Serikali kuweka saini
mikataba na kampuni za kimataifa za
Petrobras Tanzania Ltd, Heritage Rukwa Tanzania Ltd na Motherland Industies Ltd
na Oktoba 2011 Serikali kusaini mikataba mingine na
kampuni
za
Ndovu Resource na Heritage Oil za Uingereza kwa ajili ya utafutaji wa
nishati ya mafuta na gesi katika kisiwa cha Songosongo na Ziwa Rukwa
huku nchi
ikiwa haina mwelekeo sahihi wa sera, sheria, mipango na usimamizi wa
sekta hizo
nyeti kwa usalama na uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Waziri
Muhongo na Katibu Mkuu Maswi wanapaswa kuendelea kuonyesha kwa maneno na
matendo tofauti yao na viongozi waliowatangulia katika Wizara ya Nishati na
Madini Waziri Ngeleja na Katibu Mkuu Jairo kwa kutoa ufafanuzi wa ziada na
kuchukua hatua zaidi vinginevyo taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa
tarehe 21 Septemba 2012 itakuwa ni mwendelezo wa kulinda udhaifu wa kimfumo
uliojikita katika Wizara hiyo na serikali kwa ujumla.
Ni vizuri
Waziri na Katibu Mkuu wakaendelea kuzingatia ushauri niliwapa bungeni kwamba
sehemu kubwa matatizo katika sekta za nishati na madini yamechangiwa na sababu
za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na
kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali wenye dhamana na watendaji wengine na
hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi;
hivyo nguvu zielekezwe katika kurekebisha hali hiyo.

Imetolewa
tarehe 4 Oktoba 2012 na:
John
Mnyika (Mb)
Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini