WMA AWASHAURI WAZALISHAJI WA ASALI

Na Mwandishi Wetu WAKALA wa Vipimo nchini (WMA), amewapa changamoto wazalishaji wa asali kufungasha kwa kutumia njia za kisasa na kutambu... thumbnail 1 summary
Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Vipimo nchini (WMA), amewapa changamoto wazalishaji wa asali kufungasha kwa kutumia njia za kisasa na kutambulisha bidhaa zao ili ziweze kukubalika katika masoko ya kimataifa.

Ushauri huo ulitolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mipango wa WMA, Moses Ntungi, wakati akiwaelezea wananchi waliotembelea Banda la WMA kwenye maonyesho ya Wiki ya Asali yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Maonyesho vya JK Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Alisema kwamba, wafanyabiashara wa asali na bidhaa mbalimbali hapa nchini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokujua kufungasha bidhaa zao kwa njia za kisasa na namna ya kutambulisha bidhaa zao kwa kwa walaji hali ambayo inaweza kusababisha bidhaa zao kukosa soko kwenye nchi zilizoendelea licha ya bidhaa zao kuwa bora.

Alisema kwamba, WMA imekuwa ikiwapa mafunzo wajasiriamali mbalimbali kuhusu namna bora ya kutambulisha bidhaa zao zilizofungwa kama kuandika utambulisho wa bidhaa, jina la kampuni au mzalishaji au mfungashaji, eneo zinakopatikana biashara hizo, uzito au ujazo halisi wa bidhaa husika na kipimo husika ikiwamo gramu au kilogramu.

Alisema kwamba, mzalishaji au mfungashaji anatakiwa kuandika tarehe ya kutengenezwa na muda wa kwisha kwa matumizi ya bidhaa husika.

‘Vile vile wakati wa kuandika maelezo ya kutambulisha bidhaa husika, mzalishaji au mfungashaji anatakiwa kutumia lugha angalau moja inayotambulika nchini mahali bidhaa zinakopelekwa, maelezo yawe wazi, rahisi kusomeka na rahisi kuonekana na mteja,” alisema.

Ntungi alisema mzalishaji anapofungasha bidhaa yake anapaswa kupima bidhaa yake kwa kutumia mizani inayofaa kupimia bidhaa husika na kisha kuandika kipimo sahihi alichotumia wakati anafungasha bidhaa hiyo.

“Kama ametumia gramu kipimo cha uzito aandike gramu, kama ametumia kipimo cha ujazo, lita, basi aandike kipimo hicho. Katika pitapita yetu kwenye mabanda ya wajasiriamali hawa wa asali, tumekuta wengine wameandika labda 500 tu na kuacha hivyo hivyo, sasa hapo mnununuzi hawezi kujua umetumia kipimo gani, cha uzito au ujazo.

“Vile vile, baadhi ya wajasiriamali hawa utakuta wametambulisha bidhaa zao kwa lugha ya kigeni, kama vile Kiingereza bila kuweka neno la Kiswahili hata moja, wakati lengo lao ni kuuza bidhaa hiyo hapa hapa nchini.

“Hivyo basi, ni vema wanapofungasha bidhaa zao, waandike lugha ambayo kule anakopeleka bidhaa itaeleweka na kama anauza hapa Tanzania akiandika Kiingereza basi aandike na Kiswahili ili watu wengi hapa nchini waweze kuelewa vyema maelezo ya bidhaa hiyo,” alisema.

Alisema WMA inawashauri wafanyabiashara watumie mizani inayofaa wakati wa ufungashaji na kwamba mfungashaji anapaswa kupima kifungashio kabla ya kufungasha bidhaa na kisha kupima kifungashio kikiwa na bidhaa tayari ili kupata uzito au ujazo halisi wa bidhaa iliyofungashwa.
Chanzo: Mtanzania