Meno ya tembo yaitesa serikali

na Ratifa Baranyikwa , Dodoma. SERIKALI imesema inafuatilia sambamba na kuchunguza sakata la meno ya tembo kontena mbili yenye thama... thumbnail 1 summary
na Ratifa Baranyikwa , Dodoma.
SERIKALI imesema inafuatilia sambamba na kuchunguza sakata la meno ya tembo kontena mbili yenye thamani ya dola milioni 3.4 yaliyokamatwa nchini China hivi karibuni.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Maliasilil na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki,  wakati akijibu hoja zilizoibuliwa na  wabunge  wakati wakichangia kuhusu maazimio mawili ya uanzishwaji wa Hifadhi ya Saanane na  marekebisho ya mpaka na upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Akizungumzia suala hilo ambalo liliibuliwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msingwa (CHADEMA), Kagasheki aliliambia Bunge kuwa meno hayo yaliyokamatwa bado hawajawa na uhakika kama ni kweli  yametoka Tanzania.
Alisema  kwa sasa wanafanya mawasiliano na Balozi wa Tanzania nchini China, kwa sababu ripoti kuhusu meno hayo bado zina utata wa yalikotolewa, kwa sababu tayari kuna taarifa zinazoonesha kuwa kati ya makontena hayo mawili , moja linasadikiwa kuwa limetoka nchini Kongo.
Kwamba kontena la pili ambalo linadhaniwa ni la Tanzania ndilo lenye utata, kwa sababu inaonekana Tanzania ilikuwa njia ya kupitisha.
Balozi Kagasheki alisema kwa sasa wanataka kujua katika kituo cha forodha wakati meno hayo yanapitishwa kina nani walikuwa zamu.
“Hapa kuna Waziri wa Mambo ya Ndani ananisikia, kuna IGP, tunataka kujua ukweli kwa sababu bado kuna utata,” alisema Kagasheki.
Awali akichangia mara baada ya kuwasilishwa kwa azimio la Bunge la marekebisho ya mpaka na upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe iliyoko mkoani Kigoma, Mch. Msingwa alisema matukio ya kukamatwa kwa meno ya tembo yanayosadikiwa kuwa ni ya Tanzania nchini China na yale yaliyokamatwa yakiwa kwenye sanduku la maiti hivi karibuni ni ya kusikitisha.
Alisema hafurahishwi kusikia meno ya tembo wa Tanzania yamekamatwa  kwani inaonesha jinsi wanavyouawa na kwamba kuyakamata tu hakusaidii na kutaka iangaliwe njia ya kuzuia jambo hilo lisitokee.
Awali akiwasilisha azimio la uanzishwaji wa  Hifadhi ya Saanane yenye ukubwa wa kilomita za mraba 2.18, linalojumuisha visiwa vya Chankende Kubwa na Ndogo  na eneo la maji linalozunguka visiwa hivyo, Balozi Kagasheki aliliomba Bunge liazimie, kwani kutatoa fursa ya manufaa ya kimazingira, kijamii na kiuchumi kwa taifa na kuyafanya maeneo hayo kutokuwa maficho ya majambazi tena kama ilivyo sasa.
Kuhusu azimio la Bunge la marekebisho ya mpaka na upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe  alisema kutatoa fursa nyingi za kimazingira na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori walio hatarini kutoweka hususan sokwe.
Kabla ya kupitishwa kwa maazimio hayo, baadhi ya wabunge waliochangia waliitahadharisha serikali kuwa makini wakati inafanya upanuzi wa hifadhi ili kukwepa migogoro na wananchi.
Chanzo: Tanzania Daima