Songea yakabili uharibifu mazingira

na Julius Konala, Songea. HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, ina mpango wa kuunda vikundi vidogovidogo vya wajasiria... thumbnail 1 summary
na Julius Konala, Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, ina mpango wa kuunda vikundi vidogovidogo vya wajasiriamali kwa ajili ya kuvianzishia mradi wa ufugaji nyuki kwenye kata zote zinazozunguka maeneo ya misitu ili kupunguza ukataji hovyo wa miti.
Hayo yalielezwa jana na Ofisa Misitu na Nyuki wa Manispaa hiyo, Robert Mgowole, alipozungumza Tanzania Daima, mjini Songea.
Alisema hatua ya kwanza kabla ya kuanza mradi huo ni kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira pamoja na ufugaji wa nyuki kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya misitu iliyo kwenye makazi wanayoishi.
Alieleza endapo zoezi hilo litafanikiwa litasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira kama vile ukataji wa miti hovyo na uchomaji wa misitu hiyo badala yake waitumie misitu kwa ajili ya utegaji wa mizinga ya nyuki ambayo itawaingizia kipato.
“Wananchi wamekuwa na tabia ya uharibifu wa misitu kwa kujikatia miti bila utaratibu na kuendesha shughuli za kilimo kwenye vyanzo vya maji pamoja na uchomaji moto katika misitu, jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa ukame wa maji,” alisema Mgowole.
Hata hivyo, alisema wataalamu wa halmashauri hiyo kupitia idara ya misitu na nyuki wanaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya kutumia majiko banifu ambayo hutumia pumba za mpunga na marandio ya mbao katika kupikia kwa lengo la kupunguza matumizi makubwa ya misitu.