Fastjet kupunguza wafanyakazi

KAMPUNI ya ndege ya FASTJET Tanzania inampango wa kupunguza wafanyakazi wake katika viwanja vya ndege vya Mwanza na Kilimanjaro. Barua il... thumbnail 1 summary
KAMPUNI ya ndege ya FASTJET Tanzania inampango wa kupunguza wafanyakazi wake katika viwanja vya ndege vya Mwanza na Kilimanjaro.
Barua iliyosambazwa hivi karibuni na wafanyakazi wa kampuni hiyo iliyoandikwa na Mkuu wa Operesheni za ardhini wa Fastjet, Tanzania Dickson Kunambi, ilisema kuwa“Ninaamini tunaweza kukutana wakati fulani kwa sababu bado mna mali za kampuni mnazotakiwa kuzirejesha. Labda kama mmeamua kubaki nazo bila kampuni kujua, vitu kama vitambulisho, funguo na makabrasha yoyote ya kampuni.”
Hatua hiyo ya hivi karibuni inaleta maswali zaidi juu ya mustakabali wa kampuni hiyo yenye mchango mkubwa kwenye uchumi tangu ilipoanzisha huduma zake miezi michache iliyopita.
“Hatuwatarajii ninyi kufanya kazi za kawaida katika viwanja hivi vya ndege kwa sababu tayari mmeshaarifiwa kuhusu kupunguzwa katika mikutano na tayari mchakato huo unaendelea,” alisema Kunambi kupitia barua hiyo.
Mmoja wa wafanyakazi alimuuliza mkuu huyo wa operesheni katika barua pepe kuwa“Mtaendeleaje kutujali sisi katika kipindi hiki? Je, sisi bado ni wafanyakazi wa Fastjet au? Kwa sababu tangu ulipokuja na uamuzi wakati wa mkutano wetu wa mwisho Dar, sidhani kuna kitu chochote tunaweza kukaa na kujadili na kukamilisha kwa wakati huu. Kwa hiyo kinachotakiwa hapa ni kampuni kufanya mpango wa haki.”
Mmoja wa wafanyakazi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema haikuwa halali wao kupunguzwa wakati biashara ndiyo ilikuwa imeboreka zaidi.
“Tumekuwa tukifanya kazi katika masharti magumu sana tukijua kwamba kampuni itatuongezea malipo wakati mambo yakiwa mazuri, lakini kilichotokea kinakera sana,” alisema.
Alipopigiwa simu kuzungumzia tuhuma hizo, Kunambi alisema alikuwa anafahamu mchakato huo ulikuwa unaendelea, lakini hakuweza kuelewa ni jinsi gani habari hizo za ndani zimeweza kuvuja.
“Ulipataje hizi habari? Haya ni mambo ya ndani ya kampuni na bado tunaendelea na mchakato. Hata hivyo mimi si msemaji wa kampuni. Unaweza kuwasiliana na kitengo cha rasilimali watu,” alisema.
Alipobanwa kutaja sababu za kampuni kupunguza wafanyakazi na idadi yao wakati inafanya vizuri katika biashara zake Kunambi alisema ni kitengo cha rasilimali watu ndicho kinafahamu idadi.

Chanzo: Tanzania Daima