Diwani aruhusu uchomaji Msitu wa Goima

HOFU ya kutochaguliwa katika uchaguzi ujao imemfanya Diwani wa Kata ya Msisi, Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, Chunga Mgalilwa (CCM), ashindw... thumbnail 1 summary
HOFU ya kutochaguliwa katika uchaguzi ujao imemfanya Diwani wa Kata ya Msisi, Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, Chunga Mgalilwa (CCM), ashindwe kuwazuia wananchi kukata na kuchoma Msitu wa Goima.
Diwani huyo alitoa kauli hiyo jana wilayani humo katika kikao cha Baraza la Madiwani wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kata yake kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2012/2013 (Julai hadi Septemba 2013).
Hatua ya Mgalilwa kutoa kauli hiyo ilitokana na tuhuma alizopewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Betty Mkwasa, kuwa anahusika kuhamasisha wananchi kutumia msitu huo kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwamo uchomaji wa mkaa na ukataji wa kuni.
Pia diwani huyo anashutumiwa kuwa kiongozi katika kamati ya watu watatu aliyoiunda na madiwani wenzake kwa lengo la kuzuia jitihada za serikali kuzuia uharibifu wa mazingira katika msitu huo.
Akijibu tuhuma hizo, Mgalilwa alikiri kuhusika katika kamati hiyo na kuongeza kuwa yeye si mwenyekiti wa kamati bali ni mjumbe na hawezi kuwakataza wananchi kutotumia msitu huo kwani katika uchaguzi ujao anaweza kukosa kura, kwakuwa wananchi hao ndio anaowategemea kumpa ushindi.
“Wananchi wa kijiji hiki wamekuwa wakitumia msitu huu kwa kipindi  kirefu bila kuingiliwa na serikali, jambo ambalo nashangaa ni kwanini serikali imeona umuhimu wa msitu huo kwa kipindi cha hivi karibuni na kuwataka wananchi waache kuutumia msitu huo,” alisema.
Hata hivyo, Mkwasa alimtaka diwani huyo kutoa ushirikiano kwa serikali katika kukabiliana na wavamizi hao, kwakuwa siku za hivi karibuni serikali ya wilaya ilipima mipaka katika msitu huo pamoja na kuweka matangazo ya kuzuia shughuli mbalimbali lakini wananchi walitoa mabango hayo ya matangazo na kuendelea na ukataji wa miti.

Chanzo: Tanzania Daima