Nyalandu atamani wimbo wa taifa wa sasa ubadilishwe na kutumika ule unaotangaza maajabu ya utalii nchini

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema anatamani wimbo wa taifa uliopo sasa ubadilishwe na kuwa ule wa ‘Tanzania, Ta... thumbnail 1 summary
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema anatamani wimbo wa taifa uliopo sasa ubadilishwe na kuwa ule wa ‘Tanzania, Tanzania, nakupenda kwa moyo wote’, kwani wimbo huo wa ‘Tanzania, Tanzania nakupenda kwa moyo wote’ unatangaza maajabu ya utalii nchini.

“Wakati mwingine natamani sana wimbo wa taifa uliopo sasa ubadilishwe na kuwa ule wa ‘Tanzania, Tanzania nakupenda kwa moyo wote.’ Wimbo huu unatangaza maajabu ya utalii ya hapa kwetu,” alisema.

Katika hatua nyingine Wizara ya Maliasili na Utalii, inakusudia kupeleka sheria mpya bungeni kwa ajili ya kuwashughulikia majangili na watu wanaojihusisha na uuzaji na usafirishaji wa meno ya tembo ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa juzi na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akizungumza kwenye kilele cha Siku ya Utalii Duniani, ambayo kitaifa ilifanyika kwenye viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza.

Waziri Nyalandu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele hicho, alisema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kudhibiti ujangili na kuongeza kuwa kuna sheria mpya inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kupata sheria mpya ya kukabiliana na majangili hao nchini.

Alikiri kuwapo kwa taarifa za kutajwa baadhi ya vigogo serikalini wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili wa wanyamapori na uuzaji wa meno ya tembo ndani na nje ya nchi na kuona yeyote atakayethibitika kujihusisha na ujangili atachukuliwa hatua za kisheria.

“Sekta ya utalii nchini ndiyo inayoongoza kuliingizia taifa pato kubwa. Tatizo la ujangili na uuzaji wa meno ya tembo bado lipo, na wizara imekusudia kupeleka sheria mpya bungeni ambayo itakuwa kiama cha majangili,” alisema Waziri Nyalandu.


Aidha, alisema mbali na sekta ya utalii kuingiza fedha nyingi kwenye pato na uchumi wa Tanzania, lakini ajira zaidi ya 200 zilizopo nchini zinahusiana na sekta hiyo, hivyo lazima iwepo sheria kali itakayodhibiti ujambazi wa wanyama.