In details: Thamani ya meno ya tembo iliyokamatwa Z`bar ni Bil 7.4, sawa na tembo 305 waliouawa

Khamisi Kagasheki   Shehena ya meno ya tembo yaliyokamatwa juzi katika Bandari ya Zanzibar ni ya mamia ya tembo na ina tham... thumbnail 1 summary
Khamisi Kagasheki
 
Shehena ya meno ya tembo yaliyokamatwa juzi katika Bandari ya Zanzibar ni ya mamia ya tembo na ina thamani ya Sh. bilioni 7.4.
Aidha, Jeshi la Polisi Zanzibar limesema kuwa Kampuni ya Island Sea Shelts Limited iliyopo visiwani humo ndiyo mmiliki wa kontena lililokuwa limesheheni magunia 95 yenye vipande 1,021 vya meno hayo kabla ya kusafirishwa kwenda katika nchi moja ya Mashariki ya Mbali ambayo haikutajwa.

Akizungumza na NIPASHE jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, hakuwa tayari kutaja idadi ya meno yaliyokamatwa, lakini alisema mmiliki wa kampuni hiyo bado hajajulikana kama ni mzawa au raia wa kigeni.

Mussa pia alisema haijafahamika kuwa mmiliki ni raia wa China kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Alisema shehena hiyo ilikuwa na vipande hivyo vyenye uzito wa kilo 2,915 zenye thamani ya Sh. bilioni 7.4.

Kamishna Mussa alisema ni mapema kujua idadi ya meno na idadi ya tembo waliouawa. “Mimi si mtaalamu wa kujua mpaka wataalamu waviunganishe,” alisema.

Hata hivyo, taarifa zilizoko kuhusu tembo zinasema kuwa kwa wastani pembe moja ya tembo mkubwa inakadiriwa kuwa na uzito wa kilo 25. Kwa uzito huo, makadirio yanaonyesha kuwa tembo 58 wameuawa ili kupatikana kwa shehena hiyo.

Kamishna Musa alisema kuwa watuhumiwa walipanga kulisafirisha kontena hilo jana kwenda nje ya nchi na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.

Alisema tukio hilo ni la tatu kutokea Zanzibar na kwamba la kwanza lilitokea miaka sita iliyopita baada ya kontena la meno ya tembo kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume.

Mussa alisema tukio la pili lilitokea mwaka jana baada ya kontena moja kukamatwa bandarini.

“Kwa kweli hili ni tukio kubwa ambalo halijawahi kutokea katika Afrika Mashariki kwa kukamatwa kiwango kikubwa cha meno ya ndovu,”alisema Kamishna Mussa.

Alifahamisha kuwa watakaobainika kuhusika katika tukio hilo watapelekwa Tanzania Bara kufunguliwa mashtaka kwa kuwa Zanzibar hakuna sheria ya uhujumu wa wanyama aina ya tembo.

Kamishna Mussa alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili akiwamo mmoja ambaye ni wakala wa bandarini.

Kwa mujibu wa Kamishna Mussa, watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa walisema kontena hilo lilipakiwa meno hayo katika mtaa wa Daraja Bovu Mjini Zanzibar.

Alisema wanatarajia mambo mengi yatafichuka baada ya kupatikana mmiliki wa kampuni hiyo na kukamilika kwa nyaraka za mzigo huo.

Novemba 2, mwaka huu, Waziri Kagasheki, akiongozana na askari polisi katika  mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam alikamata raia watatu wa China wakiwa na pembe za tembo 706, idadi hiyo ni sawa na tembo 353, huku thamani yake ikiwa ni takribani Sh. bilioni 5.4.

 ‘MAJANGILI WAMEWEKEZA’

Wakati wanyama wakiwamo tembo kutoka hifadhi na mapori ya akiba mbalimbali nchini wakiendelea kupotea kwa kuuawa na majangili, imeelezwa kuwa wahalifu hao wamewekeza kwenye biashara hiyo haramu.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori nchini, Jonh Muya, alipokuwa akizungumza na gazeti hili.

Muya alisema majangili wamewekeza kwenye biashara hiyo haramu kama ilivyo kwa wale wanaojihusisha na dawa za kulevya, kwani imevuka mipaka ya nchi na mtandao wake ni mkubwa, ndiyo maana imekuwa ikileta shida katika kukabiliana nayo.

Kwa mujibu wa Muya, matajiri ndiyo wahusika wakuu wa vitendo vya ujangili huku wakiwatumia wananchi wa kawaida kwa ajili ya kuwachukulia mizigo yao kutoka kwenye hifadhi au mbuga.

Akizungumzia tukio la juzi la kukamatwa kwa meno ya tembo Zanzibar, Muya alisema matatizo hayo pia yanachangiwa na uwapo wa bandari bubu nyingi  katika ukanda wa Bahari ya Hindi huku zikikosa udhibiti.

Alisema, kuanzia Bandari ya Tanga hadi ya Dar es Salaam, kuna takribani bandari bubu 46, ambazo husababisha udhibiti wa vitendo vya ujangili kuwa mgumu.

Alisema kutokana na hali hiyo, inawawia vigumu hata kujua bandari ipi ambayo meno yalipitishwa hadi kwenda kukamatwa Zanzibar.

Muya aliongeza kuwa miongoni mwa vikwazo katika kukabuiliana na ujangili nchini ni ukosefu wa teknolojia ya kisasa.

Hata hivyo, alisema kwa sasa wana mipango mbalimbali katika ya kukabiliana na vitendo hivyo.

Baadhi ya mipango hiyo ni kuwa na vifaa vya kisasa yakiwamo maboti na kushirikiana na nchi nyingine ili kupeana uzoefu wa namna wanavyokabiliana na ujangali katika nchi hizo.
CHANZO: NIPASHE