Uwanja wa ndege Songwe-Mbeya kuwa kitovu cha usafiri wa anga Afrika Mashariki na Kati

Serikali imeweka wazi mpango wake wa kuufanya uwanja wa ndege wa Songwe jijini Mbeya kuwa kitovu na kiungo muhimu cha usafiri wa anga kwa ... thumbnail 1 summary
Serikali imeweka wazi mpango wake wa kuufanya uwanja wa ndege wa Songwe jijini Mbeya kuwa kitovu na kiungo muhimu cha usafiri wa anga kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dr. Shaban Mwinjaka akizindua rasmi safari za ndege ya fastjet kati ya Dar es Salaam na Mbeya

Katibu Mkuu wa Wizara ya uchukuzi, Dr. Shaban Mwinjaka amebainisha mipango hiyo ya serikali wakati akizindua safari mpya ya shirika la ndege la fastjet kati ya Dar es Salaam na Mbeya.

“Kuzinduliwa kwa safari za ndege za fastjet ni hamasa ya kutekeleza na kutimiza mipango yetu ya kuufanya Uwanja wa ndege wa Songwe kuwa kitovu cha usafiri wa ndege kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati” anasema Dr. Mwinjaka

Mgeni rasmi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dr. Shaban Mwinjaka akikata keki kuashiria kuzindua safari za fastjet kati ya Dar es Salaam na Mbeya, kushoto ni Meneja Biashara wa fastjet-Tanzania, Jean Uku 

Anasema fastjet itarahisisha uunganishaji wa safari za kimataifa kwa watu wanaotoka nchi jirani na Tanzania na kulifanya jiji la Mbeya kuwa kituo muhimu katika usafiri huo.

Mikakati hiyo ya serikali inaungwa mkono na mipango ya hivi karibuni ya fastjet ya kuanzisha safari za ndege kati ya Dar es Salaam kwenda Uganda, Kenya, Zambia, Zimbabwe, Malawi na Msumbiji ambapo tayari fastjet imeshafanikiwa kuanzisha safari ya kimataifa kati ya Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini

Novemba mosi 2013, fastjet imeongeza idadi ya mikoa na vituo inavyofanya safari zake za ndege za ndani ya nchi kwa kuzindua rasmi safari yake kati ya Dar es Salaam na Mbeya wakati mikoa ya awali ilijumuisha Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar.

 Meneja Biashara wa fastjet-Tanzania, Jean Uku akifafanua jambo

Afisa Biashara wa fastjet Jean Uku anasema kuwa uzinduzi wa safari hiyo utawawezesha wananchi wa kada mbalimbali kusafiri kwa kutumia saa moja kutoka Dar es Salaam na kutua kwenye ardhi ya Uwanja wa Songwe jijini Mbeya kwa nauli ndogo.


Jambo ambalo anaimani kuwa litarahisisha usafiri na kuwapa fursa watu wengi kusafiri na fastjet ambayo itakuwa ikifanya safari yake hiyo mara tatu kwa wiki, siku za jumatatu, jumatano na ijumaa.