Mbuga ya wanyama Kenya yafungwa vifaa maalumu vitakavyowawezesha watalii kufanya utalii kwa njia ya mtandaoni

Watumizi wa mtandao sasa wanaweza kutalii mbuga ya kitaifa ya wanyama ya Samburu nchini Kenya bila kufunga safari ya kuzuru taifa hilo. ... thumbnail 1 summary
Mbuga ya wanyama ya SamburuWatumizi wa mtandao sasa wanaweza kutalii mbuga ya kitaifa ya wanyama ya Samburu nchini Kenya bila kufunga safari ya kuzuru taifa hilo.

Hii ni baada ya kampuni ya Google kuingiza mbuga hiyo kwenye huduma ya Street View, inayowezesha mtu kutazama kwa kina eneo fulani kutoka pande zote yaani kwa digrii 360.
Mradi huo uliofanikishwa kwa pamoja na shirika laSave the Elephants, unalenga kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori.

Lengo la mradi huo pia ni kuonyesha maisha ya familia za ndovu wanaoishi kwenye mbuga hiyo.

Gari la Google Street View lilizuru na kupitia mbuga hiyo Februari 2015, na hivyo kuondoa wasiwasi kwamba huduma hiyo huenda ikatumiwa na wawindaji haramu kuwawinda ndovu kwani picha zinazoonyeshwa ni za wakati huo.

Wapiga picha walifuata barabara zinazopitia ndani ya mbuga hiyo yenye ukubwa wa kilomita 165 mraba na hawaruhusu mtu kuona yaliyomo mbali na barabara.

Ndovu, pundamilia na chui wanaonekana kwenye picha hizo kando mwa barabara.
Bodi ya Utalii Kenya inasema hiyo ndiyo mbuga ya kwanza Kenya kuwekwa mtandaoni kwa njia hiyo.

"Matumaini yetu ni kuwa kwa kufikisha Street View hapa Samburu, tutawasisimua watu pande mbalimbali duniani kukumbatia ndovu,” afisa wa Google Kenya, Farzana Khubchandani amenukuliwa akisema na shirika la habari la AFP.

Gavana wa kaunti ya Samburu, Moses Lenolkulal, pia alihudhuria uzinduzi huo.
Familia mbili kuu za ndovu zinazoonekana kwenye Street View ni Harwoods na Spice, familia ambazo huweza kutofautishwa kutokana na umbo la pembe zao.

Mkuu wa shughuli za nyanjani wa Save the Elephants David Daballen aliandika kwenye blogu katika Google kwamba anaweza kuwatambua zaidi ya ndovu 600 kwenye picha hizo.
Chanzo: BBC Swahili