WAREMBO MISS UTALII DOM WAASWA

na Danson Kaijage, Dodoma WASHIRIKI wa mashindano ya Miss Utalii, wametakiwa kuhakikisha wanatunza maadili wawapo katika kambi zao za mazo... thumbnail 1 summary
na Danson Kaijage, Dodoma
WASHIRIKI wa mashindano ya Miss Utalii, wametakiwa kuhakikisha wanatunza maadili wawapo katika kambi zao za mazoezi badala ya kujirahisisha kwa walimu na majaji.
Rai hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Island Promotion, Nyanza Hassan Lydenge, ambao ndio waandaaji wa Miss Utalii Mkoa wa Dodoma.
Alisema kuwa, kushiriki mashindano kama hayo, siyo tiketi ya kuonesha utovu wa nidhamu bali inatakiwa kuzingatiwa misingi bora na yenye maadili, ambayo yanaonyesha utamaduni wa Mtanzania.
“Wapo watu wamekata tamaa ya kushiriki katika mashindano ya ulimbwende kutokana na baadhi ya washiriki kuonyesha tabia ambazo siyo nzuri kwa walimu wao ama waamuzi, ambao ushiriki katika mashindano hayo.
“Washiriki wa mashindano ya Miss Utalii kote nchini, lazima watambue kuwa, mashindano hayo siyo sehemu ya kufanyia mambo yao ya ovyo, bali ni sehemu ambayo inawakilisha nchi kwa kutangaza vivutio ndani na nje ya nchi,” alisema Lydenge.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, taratibu za kuwapata washiriki hao, zilifuatwa ikiwamo kutangaza na kutoa fomu kwa wale ambao wangependa kujiunga na mashindano hayo, ambako walijitokeza warembo 35 na kufanyiwa usaili na kubaki 16.
Alisema kuwa, hatua ya maandalizi ya Miss Utalii Dodoma, wamewashirikisha viongozi wa ngazi ya mkoa, ili kuhakikisha zoezi hilo linaendeshwa katika maadili ambayo yanamruhusu mshiriki kufanya vizuri.
Lydenge alisema warembo wanatarajiwa kuingia kambini rasmi Oktoba 13 kujiwinda na kinyang’anyiro hicho.
Malkia wa Miss Utalii Dodoma atajinyakulia sh milioni 1, wa pili sh 750,000 mshindi wa tatu ataondoka na sh 500,0000 wakati atakayeshinda nafasi ya vipaji atapata sh 250,000 na watakaosalia watapata kifuta jasho cha sh 100,000 na vyeti vya ushiriki kila mmoja.
Chanzo: Tanzania Daima