NEMC YAITOZA MIL. 10 CORAL HOTEL

na Betty Kangonga MMILIKI wa Hoteli ya Coral ya jijini Dar es Salaam ametakiwa kulipa fidia ya sh milioni 10 kwa kuharibu mazingira ya viu... thumbnail 1 summary
na Betty Kangonga
MMILIKI wa Hoteli ya Coral ya jijini Dar es Salaam ametakiwa kulipa fidia ya sh milioni 10 kwa kuharibu mazingira ya viumbe wa baharini, huku akipewa siku 7 kuondoa kifusi cha mchanga kilichojazwa katika eneo la ufukwe wa bahari ya Hindi.
Akizungumza wakati alipotembelea eneo hilo, Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Manchare Suguta, alisema kuwa mmiliki huyo amekiuka utaratibu na kuamua kufanya ukaushaji wa bahari kinyume na sheria.
Suguta alisema kuwa kibali kilichotolewa na NEMC kwa mmiliki huyo ni kwa ajili ya kujenga ukuta wa matundu wa mita moja na upana mita moja, lakini badala yake akaamua kuongeza kifusi sehemu asiyotakiwa hatua inayoashiria kuvunja makubaliano ya awali.
Alisema kuwa hatua iliyofanywa na mmiliki huyo ni kosa kwa kuwa NEMC haijawahi kutoa kibali kingine cha kujaza kifusi katika ufukwe huo, hivyo alimtaka kufika katika ofisi za NEMC ili kulipa faini hiyo.
Suguta alisema kuwa kutokana na hilo akamtaka mkandarasi mshauri wa ujenzi huo kuhakikisha anafuata maelekezo na kusimamia kwa dhati sheria za ujenzi katika fukwe za bahari.
Mkandarasi anayesimamia ujenzi wa ukuta huo, Donald Mpenihaka, alisema kutokana na maelezo ya NEMC mmiliki huyo atakuwa amefanya kosa.
Awali Mkurugenzi wa Coral Hotel, Kelvin Patel, alibishana na mwanasheria wa NEMC hadi pale mkandarasi alipoamua kuingilia kati na kumtaka kukubali kosa hilo.
Chanzo: Tanzania Daima