50 wakamatwa kwa ujangili, wamo watumishi wa serikali

ZAIDI ya watu 50 wakiwemo watumishi wa serikali, wamekamatwa na katika operesheni ya kitaifa ya kusaka wawindaji haramu na kufikishwa katik... thumbnail 1 summary
ZAIDI ya watu 50 wakiwemo watumishi wa serikali, wamekamatwa na katika operesheni ya kitaifa ya kusaka wawindaji haramu na kufikishwa katika mahakama ya wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Watuhumiwa hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti na kikosi hicho katika mikoa ya Simiyu, Manyara, Mara na ndani ya hifadhi ya taifa ya Serengeti.

Kesi za washitakiwa hao zimesajiriwa jana katika mahakama ya wilaya ya Bunda, mbele ya mahakimu Safina Simufukwe na Hamadi Kasonso.

Waendesha mashitaka wa serikali Halili Nuda na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Barasa, pamoja na mwanasheria wa Tanapa, Emmanuel Zumba, wamewasomea mashitaka hayo washitakiwa hao.

Imeelezwa kuwa washitakiwa hao kwa nyakati na maeneo tofauti walikamatwa na kikosi hicho wakiwa na nyara za serikali kinyume cha sheria.

Aidha, imeelezwa kuwa washitakiwa hao baadhi yao walikamatwa na pembe za wanyama, nyama mbichi na nyama kavu kinyume cha sheria.

Washitakiwa hao wanashitakiwa kwa makosa ya kuingia hifadhini, kukutwa na nyara za serikali na kuendesha uwindaji haramu kinyume cha sheria, ambapo wote wamekana mashitaka yao.

Watumishi wa serikali waliokamatwa na kikosi hicho wamo waajiriwa wa Tanapa, ambapo baadhi yao wamedhaminiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana na wengine wakipelekwa mahabusu.

Kesi hizo zimehairishwa, ambapo zitatajwa tena mahakamani hapo.

Operesheni hiyo ya kitaifa inashirikisha vyombo mbalimbali vya dola, wakiwemo wanajeshi wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ).