Kagasheki amfikisha RCO kwa IGP

  PICHANI: MHE. BALOZI HAMIS KAGASHEKI AKISISITIZA JAMBO JUU YA ORERESHENI TOKOMEZA INAYOENDELEA NCHINI KWA WAANDISHI WA HABARI (HAWAPO ... thumbnail 1 summary
  PICHANI: MHE. BALOZI HAMIS KAGASHEKI AKISISITIZA JAMBO JUU YA ORERESHENI TOKOMEZA INAYOENDELEA NCHINI KWA WAANDISHI WA HABARI (HAWAPO PICHANI), MAKAO MAKUU YA WIZARA HIVI KARIBUNI.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema kuwa suala la Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha (RCO), Duwan Nyanda, anayetuhumiwa kutorosha watuhumiwa wa ujangili linashughulikiwa na Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema. Anaripoti Grace Macha wa Tanzania Daima, Arusha

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kagasheki alimtuhumu RCO huyo kuhujumu operesheni ‘Tokomeza Majangili’, baada ya kudaiwa kuwatorosha majangili wawili raia wa kigeni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Arusha, Kagasheki alisema kuwa vita dhidi ya ujangili wa meno ya tembo inayotishia kutoweka kwa wanyama hao haitakoma mpaka majangili hao waache.

Aliongeza kuwa watumishi wa serikali wanaowasaidia majangili hao wanasukumwa na ubinafsi kwa kuamua kujinufaisha binafsi na rasilimali hizo za umma.

Alisema operesheni hiyo ya ‘Tokomeza Ujangili’ iliyoanza hivi karibuni inahusisha majeshi yote ya ulinzi na usalama.

RCO Nyanda anadaiwa kusaidia kuwatorosha watu wawili wenye uraia wa Saudi Arabia ambao walikuwa wakishikiliwa baada ya kukutwa wakiwa na silaha na baadhi ya vithibitisho vinavyoonesha walikuwa majangili.

“Inasikitisha sana na inaturudisha nyuma ikiwa kama kiongozi wa jeshi anayevaa sare ya Watanzania, kwa makusudi anawaachia watuhumiwa wa ujangili na kusaidia kuondoka nchini,” alisema Kagasheki wakati akizungumza na waandishi mwishoni mwa wiki.

Alisema katika tukio hilo, polisi walifanikiwa kuwakamata watu hao wakiwa na vithibitisho vyote vya kujihusisha na ujangili na kuwapeleka kituo cha polisi Arusha kwa ajili ya mahojiano.

Alifafanua kuwa kabla ya kuwekwa rumande, watu hao walinyang’anywa hati zao za kusafiria ili kuwazuia wasitoroke. Lakini katika hali ya kushangaza RCO Nyanda alihakikisha anawatoa nje kwa dhamana na kisha aliwakabidhi hati hizo kitu kilichosababisha watoroke nchini.

Mapema akifungua mkutano wa mwaka wa Chama cha Mashirika ya Utangazaji ya Kusini mwa Afrika (Saba) jijini hapa jana, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alivitaka vyombo vya habari vya nchi hizo kujikita katika kutangaza vivutio vilivyopo.

Alisema lengo ni kuongeza idadi ya watalii watakaovutiwa kuvitembelea ili kukuza uchumi wa nchi zao.

Pia vimetakiwa kuandaa vipindi vya maendeleo ikiwamo kutangaza vivutio vya kiutamaduni ambapo mbali na kuyaingizia mapato mataifa yao kutawezesha kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa maeneo husika.

Alisema kuwa vyombo vya habari ni muhimu katika kuelimisha na kuburudisha lakini vikitumiwa vizuri vinaweza kuchangia kuleta maendeleo ikiwamo sekta ya utalii.

Dk. Bilal alisema suala la kutangaza vivutio vya Afrika lisiachiwe vyombo vya habari vya nje ya bara pekee ambavyo huwashawishi watalii kwenda maeneo wanayoyataka wao, bali vitangaze maeneo yote kwa kueleza uzuri wake.

Alivitaka vyombo hivyo kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa uhifadhi na ulinzi wa vivutio vya maliasili badala ya kusubiri ziharibike ndipo vianze kutoa taarifa za madhara.

Dk. Bilal alivitaka vyombo vya habari nchini kuungana na serikali katika kukabiliana na ujangili ili kuhakikisha unamalizika kabisa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa), Allan Kijazi, alisema tayari wamekamilisha taratibu za Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mawasiliano nchini (TCRA) ili waruhusiwe kuandaa filamu za wanyamapori.

Alisema kuwa kwa sasa ni watu kutoka mataifa ya Ulaya ndio hufika kwa ajili ya kuandaa filamu hizo, hivyo kukamilika kwa taratibu ni fursa kwa shirika hilo kuanza kuandaa filamu hizo zikionesha na kuzungumzia vivutio vyote vya utalii vilivyoko nchini.

Kijazi alisema kwa sasa ni vivutio vichache tu ndivyo vinavyotambuliwa huku vingi vikiwa vimeachwa, jambo alilotaka kuwepo na mwamko miongoni mwa wanahabari kuvitangaza kwa kufuatilia ni kitu gani kipya kinaendelea kwenye sekta ya utalii na kuvitangaza kwa usahihi.

Mkutano huo wa siku nne unahudhuriwa na washiriki kutoka nchi 14 za SADCC, ambapo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa.