Operesheni ya kusaka nyara na silaha yaleta kilio, Polisi wadaiwa kumpiga risasi kiziwi

Mtu mmoja ambaye ni bubu na kiziwi, mkazi wa Kijiji cha Bisarara Kata ya Sedeco wilayani Serengeti, amelazwa katika Hospitali Teule ya Ny... thumbnail 1 summary
Mtu mmoja ambaye ni bubu na kiziwi, mkazi wa Kijiji cha Bisarara Kata ya Sedeco wilayani Serengeti, amelazwa katika Hospitali Teule ya Nyerere akidaiwa kupigwa risasi na askari waliokuwa wakiendesha operesheni ya kusaka nyara na silaha.
Habari ambazo zimethibitishwa na polisi Mkoa wa Mara,uongozi wa kata na Hospitali Teule ya Nyerere zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 9,mwaka huu kati ya saa 8.30 hadi 11 alfajiri kijijini hapo.
Mganga wa zamu katika hospitali hiyo, Nyanzirali Kitara amethibitisha kumpokea majeruhi huyo Mnanka Machumbe Nyangige(18)ambaye amelazwa katika kitanda namba 5 wodi ya wanaume .
Naye mganga aliyemfanyia vipimo, Tanu Warioba alisema taarifa kamili ya ukubwa wa majeraha itatolewa baadaye.
Jitihada za kuwasiliana na majeruhi huyo hazikufanikiwa kutokana na ulinzi wa askari polisi. Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa watu wanaomwuguza majeruhi huyo, mkazi wa kijijini hapo, Joseph Ryoba Maseke(18), alisema kundi kubwa la askari walivamia kijijini hapo wakisaka silaha na majangili wa tembo.
“Walivamia mji huo na kubomoa milango, wakaingia ndani wakawa wanaamuru watu wajisalimishe...lakini huyu majeruhi ni bubu na kiziwi akawa hasikii …walichofanya ni kumfyatulia risasi na kumjeruhi ndipo akurupuka na kuanguka nje,” alisema.
Alisema baada ya kumjeruhi waliendelea kupiga watu ovyo wakiwamo wanawake, wakidai wanataka bunduki, kumchukua mwenye mji huo Machumbe Nyangige na vijana wake wawili Nyangige na Mwita kwenda nao polisi.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Fernandi Mtui akizungumza kwa simu alikiri kutokea tukio hilo: “Nimeambiwa na nimewaagiza kufuatilia kujua aliyepigwa risasi ni nani… kapigwa na nani… ilikuwaje… mazingira hayo kisha wanijulishe ana mimi nitawajulisha,” alisema.
Chanzo: Mwananchi