Mashirika yaungana kutekeleza kampeni ya kulinda ardhi ya mwanamke

Dotto Kahindi Kidole kimoja hakivunji chawa! Ni msemo wa siku nyingi ambao unabainisha umuhimu wa kushirikiana katika kulitekeleza jamb... thumbnail 1 summary
Dotto Kahindi

Kidole kimoja hakivunji chawa! Ni msemo wa siku nyingi ambao unabainisha umuhimu wa kushirikiana katika kulitekeleza jambo fulani ili liweze kuwa na ufanisi zaidi. 

Usemi huu ndio umeyaibua mashirika na taasisi mbalimbali nchini Tanzania na kuungana kwa pamoja katika kutekeleza kampeni ya Linda Ardhi ya Mwanamke. 

Kampeni hiyo itakayozinduliwa Novemba 21, 2019, jijini Dar es Salaam inalenga kukuza uelewa wa jamii juu ya haki ya mwanamke katika kumiliki ardhi ili kufanikisha ushiriki wake kwenye maendeleo endelevu.

Mwanasheria wa Landesa Tanzania, Geofrey Massay akita mada wakati wa semina ya waandishi wa habari

Mwanasheria wa Landesa Tanzania, Geofrey Massay anasema, malengo ya maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa endapo mwanamke ataachwa nyuma katika masuala muhimu ikiwemo umiliki wa ardhi. 

“Bila ardhi kwajili ya shughuli mbalimbali hasa za kiuchumi ni jambo gumu mwanamke kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu kufikia 2030” anasema Massay.

Lakini kwanini mashirika haya yanakusudia kushirikiana katika kutekeleza kampeni hii ya Linda Ardhi ya Mwanamke? 

Mchambuzi wa masuala ya ardhi, Khadija Mrisho anasema zipo sababu nyingi lakini kubwa ni kukusanya nguvu ya pamoja ya kuwafikia watu wengi nchini ili kuleta mabadiliko chanya.

“Tumefanya shughuli nyingi za mambo ya haki za mwanamke katika kumiliki ardhi lakini hapakuwa na kampeni ya pamoja inayojumuisha mashirika mengi kuelimisha jamii juu ya suala hili” anasema Khadija


Mbali na mashirika hayo kushirikiana katika kampeni hiyo, waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali nao wamealikwa kushiriki katika kampeni hiyo.

Mmoja wa Wakurugenzi wa Bodi ya Landesa, Edda Sanga anasema, waandishi wakitumia kalamu zao kwa ubunifu na maarifa kampeni hiyo itakuwa rahisi kufanikiwa na kuwafikia watu wengi.

Hata hivyo anatoa angalizo kwamba, ni lazima waandishi hawa wawe na uelewa wa kutosha kwenye suala zima la umiliki wa ardhi kwa wanawake na njia bora ya kufikisha ujumbe huo kwa jamii.

“Kampeni hii sio rahisi kama mnavyoifikiria, ni ngumu na inahitaji uelewa wa kutosha, ubunifu na maarifa katika kufikisha ujumbe kwa jamii husika” anasema Sanga.