MADINI SASA YAANZA KUTOROSHWA KWA KUTUMIA PUNDA

  Mkokoteni unaovutwa na Punda WIZARA ya Nishati na Madini imegundua ‘madudu’ katika sekta ya madini, iki... thumbnail 1 summary
 Mkokoteni unaovutwa na Punda
WIZARA ya Nishati na Madini imegundua ‘madudu’ katika sekta ya madini, ikiwamo utoroshaji wa madini ya tanzanite kwa punda na ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na kampuni za migodi nchini.
Kutokana na hilo, imefanya marekebisho ya mifumo ya ulipaji kodi iliyowezesha kulipwa kwa baadhi ya madeni na imetangaza Mtanzania yeyote, ikiwamo mfanyakazi wa mgodi atakayetoa taarifa za utoroshaji wa madini, atapewa asilimia 30 ya thamani ya mzigo utakaokuwa umetoroshwa.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza katika uzinduzi wa Kitabu cha Ripoti inayohusu Haki za Binadamu katika Kazi, Biashara, Mazingira, Ardhi, Ulinzi na Haki ya Mlaji.
Hafla hiyo iliandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na yeye alikuwa mgeni rasmi.
Akizungumza kabla ya uzinduzi wa ripoti hiyo iliyoelezea ukiukwaji mkubwa wa haki za wafanyakazi katika kampuni za madini nchini na uharibifu wa mazingira uliobainika, Masele alikubaliana nayo na kueleza jinsi Serikali ilivyojipanga kukabiliana na kadhia hiyo.
“Kuna ‘madudu’ mengi na makubwa yanafanyika, rasilimali za nchi hii zinatoroshwa na kuyeyuka, tumegundua kule Manyara madini pekee yanayopatikana Tanzania tu ulimwenguni kote-tanzanite yanatoroshwa kwa punda, hii haiwezekani kukaa kimya, wezi wa mali zetu ni Watanzania wenyewe, tubadilike,” alisema Masele na kuongeza: “Kuna watu wanapewa asilimia 10 ya madini yanayotoroshwa, tumegundua hilo pia sasa tumesema mwananchi au mfanyakazi atakayegundua utoroshaji na kutoa taarifa kwetu, tutampa asilimia 30 ya fedha ambayo ni thamani ya mali aliyookoa”.
Akisisitiza ukwepaji kodi, alisema: “Tena nitoe onyo kwa kampuni zinazokwepa kodi na kukiuka haki za binadamu hasa katika sekta inayosimamiwa na wizara yetu, waache mara moja maana kuna mapinduzi makubwa yanafanyika sasa na hatutasita kuyafutia leseni mara moja”.
Masele alisema walibaini kampuni zote za madini nchini zikikwepa baadhi ya kodi kupitia uandikaji wa nyaraka zao na sasa wamezibaini na kuanza kulipa madeni hayo.
Alitoa mfano kampuni ya Barrick katika ukokotoaji wa hesabu, ilibainika kuwa na deni la zaidi ya Sh bilioni 5.6 na hadi sasa imelipa Sh bilioni 2.3; nyingine ni TanzaniteOne inayodaiwa zaidi ya dola za Marekani milioni 2.5.
“Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) ilikuwa inadaiwa zaidi ya dola milioni 1.4 ambazo sasa imeanza kuilipa Halmashauri ya Geita, niseme tu kuna mapinduzi makubwa na tunaamini Watanzania wako nyuma yetu hatuogopi,” alisema Masele.
Kuhusu TanzaniteOne, alisema leseni yake imekwisha tangu Agosti na Serikali imesitisha kuipa leseni nyingine mpaka mpango wa kurejesha asilimia 50 ya hisa serikalini ili kuondoa umiliki binafsi uliopo sasa na masuala mengine ya utendaji vitakapokaa vizuri.
Alisema katika kuhakikisha kuna usimamizi mzuri wa kodi na rasilimali za madini, mafuta na gesi nchini, Wizara inafanya mapinduzi makubwa katika taasisi zake kwa kufumua Bodi, kupanga mifumo na kuongeza nguvu ya kiutendaji ya rasilimali watu.
Masele alisema miongoni mwa Bodi zitakazofumuliwa ni pamoja na ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ili kuongeza usimamizi katika sekta ya madini, pia itafanya marekebisho makubwa ya utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC).
Alisema lengo la wizara ni kutekeleza malengo ya kiuchumi ya mwaka 2020 hadi 2025 ya nchi kuwa katika uchumi wa kati kwa kutumia rasilimali zake hasa madini, gesi na mafuta na kusisitiza kuwa hawataacha kuwachukulia hatua wezi wa rasilimali, waharibifu wa mazingira na ardhi.
Alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wanaharakati wa haki za binadamu, kwamba Serikali inawatambua na haipingi kukosolewa, lakini kwenye pongezi ipewe, huku akiwahakikishia kuwa utafiti wao ni moja ya zana za kuendeleza utendaji unaoendelea hivi sasa katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwa kuonesha matumaini mapya kwa wananchi, hasa usalama wao katika maeneo ya kazi kwenye migodi na kampuni za uwekezaji.
Kuhusu ripoti ya utafiti, Kijo- Bisimba alisema utafiti ulifanyika nchi nzima na kugundua ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wafanyakazi wa migodini, ujira mdogo na usalama kazini, uharibifu wa mazingira na ardhi.
“Ilizoeleka katika nchi nyingi, kwamba walaumiwa wa ukiukaji wa haki za binadamu ni Dola, lakini sasa hali hiyo imebadilika, sekta binafsi inashiriki katika ukiukaji wa haki za binadamu kupitia mifumo yao ya utendaji na kukwepa kulipa kodi,” alisema Dk Kijo-Bisimba.
Akitoa takwimu, Wakili na Mratibu wa Uwajibikaji wa Kampuni na Mazingira wa LHRC, Flaviana Charles alisema wafanyakazi asilimia 15.77 waliohojiwa walikiri kuwapo na ukiukwaji wa haki za binadamu migodini na ujira mdogo, hakuna haki ya kujumuika (kuwa na vyama vya wafanyakazi).
“Pia asilimia 28.22 ya kampuni hazina sera ya kuzuia ajira kwa watoto na asilimia 4.62 ya kampuni hazishirikishi wananchi kuchukua ardhi ya uwekezaji, pia watu hawajui haki zao wanapouziwa bidhaa bandia,” alisema Charles.
LHRC waliiomba Serikali kuhakikisha pia kuwa familia 20 zinazoishi katika mahema Geita zilizopisha mradi wa GGM, zinajengewa nyumba. Naibu Waziri Masele alisema tayari GGM imekubali kujenga nyumba hizo.
Kwa mujibu wa LHRC, utafiti huo ni wa kwanza wao kuufanya nchini kuhusu masuala ya haki za wafanyakazi, mlaji, ardhi, mazingira na ulinzi.