Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda akiwasisitizia wahitimu na wageni
(hawako pichani) waliofika katika mahafali ya kwanza na ya pili ya Chuo cha
Ufugaji Nyuki Tabora kuwa serikali lazima ijenge Chuo KIkubwa Cha Ufugaji Nyuki
Tabora.
Na
Tulizo Kilaga, Tabora
SERIKALI imeahidi kujenga chuo kikubwa cha
mafunzo ya ufugaji nyuki katika eneo la Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki
mkoani Tabora ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya kwanza Barani Afrika
katika uzalishaji wa mazao yatokanayo na nyuki.
Ahadi hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na
Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda aliyekuwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya kwanza
na ya pili ya Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji nyuki Tabora alipokuwa akiwahutubia
wahitimu kabla ya kuwatunuku vyeti na zawadi.
Mhe. Pinda alisema pamoja na mapungufu ya
chuo hicho yaliyotokana na tabia ya kuhamisha mafunzo yake mara kwa mara kwenda
kwenye vyuo mbalimbali vya Wizara ya Maliasili na utalii nchini, chuo kina
umuhimu mkubwa kutokana na kuwa ni chuo pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki
na Kusini mwa Afrika.
“Siku za nyuma chuo kiliweza kupata watu
kutoka nchi za nje kuja kujifunza, hivyo serikali haiwezi kukiacha solemba!
Kama tumeweza kujenga Chuo kikubwa cha Serikali za Mitaa, Hombolo
kinachotufanya tushindwe kujenga chuo kikubwa hivi ni nini? Kwamba
hatuoni thamani yake? Si kweli, miaka kumi ijayo thamani yake itaonekana tu,”
alisema Mhe. Waziri Mkuu.
Aliongeza kuwa, tatizo la kutoendelezwa kwa
chuo hicho wakati mwingine kunatokana na viongozi kutojua kinachoendelea, hivyo
aliomba uongozi kuwakilisha mpango mkakati wake ili serikali iweze kuipembua na
kuona wapi pakuanzia.
Aidha, Mhe. Pinda aliipongeza Wizara ya
Maliasili na Utalii kwa uamuzi wake wa kukirudisha Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji
Nyuki mkoani Tabora na kutoa onyo kwa yoyote atakayetaka kujaribu kukihamisha
tena kutofanya hivyo ili serikali iweze kujipanga na kusonga mbele.
Aliongeza kuwa, Tanzania ina hifadhi za
misitu na maji ya kutosha inayotoa fursa ya kuzalisha asali nyingi, hivyo
amewaasa wananchi kuchangamkia fursa hiyo ili kuiwezesha nchi kushika namba
moja kwa nchi za Bara la Afrika zinazozalisha asali.
“Tanzania hivi sasa inapitwa na Ethopia kwa
uzalishaji asali, nchi ambayo haina misitu yakutosha, hili haliwezekani
tuangalie mpango mikakati yetu. Ufugaji asali hauhitaji mtaji mkubwa, na soko
lake ni la uhakika, tumshinde Ethiopia na hili linawezekana kama tutapanua
mawazo yetu juu ya sekta hii,” alisema Mhe. Pinda.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, alimshukuru Waziri Mkuu kwa moyo wake
wakusimamia kidete sekta ya ufugaji nyuki nchini na kutoa fursa za ajira kwa
wananchi wengi.
Aidha, Mhe. Pinda alisisitiza kiu yake ya
kuona Tanzania inazalisa asali nyingi kwa kuwaahidi wahitimu kuwapa zawadi ya
mizinga 100 endapo wataunga na kuunda kikundi cha ufugaji nyuki na kutumia
elimu waliopata kuweza kujipatia kipato.
Katika kusisitiza hilo Mkuu wa Mkoa wa
Tabora, Bi. Fatma Mwasa naye aliwahidi wahitimu ambao ni wakazi wa mkoa wake,
kuunda vikundi vya watu waiopungua kumi kwa kikundi ili aweze
kuwapatia mtaji wa mizinga.