Maafande 2 wanaswa wakiuza jino la tembo

Polisi wawili wa Kitengo cha Upelelezi katika Kituo cha Polisi Mugumu wilayani Serengeti wakishirikiana na raia wawili, wamekamatwa na ki... thumbnail 1 summary
Polisi wawili wa Kitengo cha Upelelezi katika Kituo cha Polisi Mugumu wilayani Serengeti wakishirikiana na raia wawili, wamekamatwa na kikosi maalumu cha ‘Okoa Maliasili’ wakijaribu kuuza jino moja la tembo.
Kukamatwa kwa askari hao kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Fernandi Mtui ambaye alidai si msemaji wa operesheni hiyo na kuwa anaendelea kufuatilia kwa kuwa wamepelekwa kwenye kambi maalumu inayotumiwa na kikosi hicho.
“Kwa kweli sijajua kwa undani ilivyotokea, naendelea kufuatilia maana hawako kwetu hao. Kama itabainika kuwa walihusika ama walikuwa kwenye kazi ya kusaidia kukamatwa kwa watuhumiwa lazima itakuwa wazi. Haya mambo hakuna kitakachofichwa”alisema kamanda.
Taarifa zilizolifika gazeti hili kutoka katika vyanzo vya uhakika, askari hao waliotajwa kwa jina moja moja la Koplo Isaack na Sixbert wa Idara ya Upelelezi walikamatwa Oktoba 25, kati ya saa 4-5 usiku eneo la Sedeco mjini Mugumu baada ya kuwekwa mtego maalumu.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo polisi zinadai kuwa askari hao wakiwa na gari aina ya Toyota Corolla yenye namba za usajili T269 BRN mali ya Sixbert walifika eneo hilo na jino hilo kwa ajili ya kuuza wakiwa na raia wawili ambao majina yao hayajajulikana ndipo wakanaswa.
Habari hizo zilisema baada ya kukamatwa watuhumiwa wote pamoja na gari walichukuliwa na kupelekwa eneo la Andajenga lililomo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambako kikosi hicho kina kambi maalumu.
Hata hivyo kuna habari zinasema kuwa kukamatwa kwa askari hao kunatokana na kuwapo kwa taarifa za kuhusika na biashara hiyo kwa kuuza vielelezo mbalimbali vinavyokamatwa na kuhifadhiwa polisi.
Tuhuma za askari polisi kujihusisha na mitandao ya ujangili kwa wilayani Serengeti zimekuwa nyingi huku baadhi ya taasisi zikibainisha ugumu wa kuwakamata watuhumiwa kwa kuwa hupewa taarifa mapema na askari walioko kwenye mtandao huo na kukimbia.
Mwanzoni mwa mwaka huu askari polisi wawili kutoka Mkoa wa Kagera walikamatwa wilayani Serengeti wakiwa na meno ya tembo kilo 18 wakidaiwa kutumiwa na mfanyabiashara kutoka Biharamulo,walifukuzwa kazi na kesi iko mahakamani.
Kukamatwa kwao hao kunafanya idadi ya askari waliokamatwa na operesheni hiyo kufikia wanne ,wawili wakiwa idara ya wanyamapori wa halmashauri hiyo.
Askari hao akiwemo Kaimu Afisa Wanyamapori Wilaya, Cathbert Boma ambaye alikutwa na meno ya tembo ofisini na Omary Rutiginga ambaye anadaiwa kukutwa na kipande cha nyama ya ngiri.
Wote wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Bunda ambako walipewa dhamana. 
Chanzo: Mwananchi