Ahadi za mabilioni ya dola zilivyoharibu majadiliano ya mkataba wa mazingira COP21, Paris, Ufaransa

Dotto Kahindi, Le Bourget, Paris, Ufaransa Mahitaji Matatu kwa nchi zinazoendelea Majadiliano yanayoendelea kwenye Mkutano wa Ki... thumbnail 1 summary
Dotto Kahindi, Le Bourget, Paris, Ufaransa

Mahitaji Matatu kwa nchi zinazoendelea
Majadiliano yanayoendelea kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Mjini Paris, Ufaransa huenda yakashindwa kuzaa matunda mema kwa nchi za Afrika kutokana na wengi wao kupoteza msimamo baada ya kutangazwa kwa mabilioni ya misaada ya mabadilko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea.

Ahadi za mabilioni hayo ya dola za kimarekani na euro zilizotolewa na mataifa yaliyoendelea yameathiri kwa kiasi kikubwa majadiliano ya mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa zimebadili fikra na msimamo wa viongozi wa nchi zinazoendelea na kuacha kudai mambo muhimu ya uwajibikaji kwa mataifa yanayoendelea kwa nchi za Afrika.

Katika andiko la tatu la mkataba wa mabadiliko ya tabianchi ambalo limetoka Desemba 10, 2015 nchi za Afrika ziliondolewa kwenye kundi la nchi zilizo kwenye mazingira magumu kwa kuathirika na mabadiliko ya tabianchi jambo ambalo linatia doa msimamo wa awali wa Afrika.

Kuondolewa kwa Afrika kwenye kundi hilo kunamaanisha kuwa Afrika itakosa misaada mingi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hasa katika kutekeleza mchango wa kila nchi katika juhudi za dunia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Intended Nationally Determined Contributions – INDCs).

Wachambuzi wa mambo wanasema ahadi hizo zimetumika kama rushwa kushawishi wawakilishi wa Mataifa ya Afrika katika mkutano huo ili wanyamaze na kuyakubali mapendekezo ya mataifa yaliyoendelea.

Katika majadiliano yaliyofanyika jana usiku, nchi za Afrika hazikusema chochote ambapo wawakilishi wao waligeuka bubu na kutikisa vichwa kuashirika kukubaliana na mapendekezo yaliyopo kwenye andiko la mkataba huo.

Wanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi wameendelea kupaza sauti zao kupinga andiko hili wanalosema halikubaliki na kwamba limejaa hadaa kubwa kwa nchi za Afrika.

“Afrika haijatambuliwa kwenye orodha ya mataifa zilizo kwenye mazingira magumu kwa kuathirika na mabadiliko ya tabianchi tofauti na ilivyokuwa kwenye andiko la awali, je kuna uwezekano wa jambo hili kubadilishwa kabla ya kupitishwa kwa andiko?” anahoji Mithika Mwenda, Mratibu wa PACJA.

Mithika Mwenda, Mratibu wa PACJA
Pamoja na nchi za kiafrika kunyamazishwa na ahadi hizo za pesa zilipaswa kutambua kuwa hizo pesa ni ahadi ambayo hata hivyo haijabainishwa wazi kwenye andiko la mkataba wa mazingira na kwamba kuna asilimia nyingi kuwa ahadi hzio hazitatekelezwa.

Ahadi zilizowatia kiwewe mataifa ya afrika na hivyo kuwaziba midomo kuchangia na kuweka shinikizo katika mambo ya msingi kwa bara hilo ni pamoja na ahadi ya Austria ya EUR 500 milioni kati ya 2015 na 2020.

Ahadi nyingine ni kama ifuatavyo, nchi na kiwango kwenye mabano Belgium (EUR 50 millioni), Canada (CAD 2.65 bilioni), Czech Republic (USD 5.3 milioni), Denmark (USD 38 milioni), Estonia (EUR 6 millioni), European Commission (EUR 2 billioni), Finland (EUR 500 Millioni), France (EUR 5 billion), Hungary (USD 4 million) wakati Germany ikiahidi kuongeza msaada wake wa sasa maradufu kufikia 2020

Ahadi nyingine ni Iceland (USD 10 million), Ireland (EUR 175 million), Italy (USD 4 billion ), Japan (Yen 1.3 trillion ), Lithuania (EUR 100 000), Luxembourg (EUR 365 million ), Netherlands (EUR 440 million ), New Zealand (NZD 200 million), Norway ( USD 400 million ), Poland (USD 8 million ), Spain ( EUR 900 million) na Uingereza (GBP 5.8 billion)

Majadiliano ya mkataba wa mabadiliko ya tabianchi bado yanaendelea ambapo andiko la mwisho linatarajiwa kutoka jumamosi ya Disemba 12, 2015 na endapo wawakilishi wa mataifa ya Afrika wataendelea kulala ni dhahiri mkataba huu utakuwa ni wenye kuyanufaisha mataifa yaliyoendelea.